Jamaa apongeza kanjo kufukuza wachuuzi wa mayai, "Nairobi inataka kuwa kama Dubai"

"Maono ya Nairobi kuwa Dubai hayana nafasi kwa wachuuzi wa vyakula vya mitaani wasio na usafi wanaouza soseji na mayai ya kuchemsha kwa toroli, ambao hata hawalipi kodi za kaunti na ushuru."

Muhtasari

• Kwa mujibu wa Njohi, jiji la Nairobi ni la wafanyibiashara wa mabilioni ya mtaji wala si jiji la kufanya biashara za kuchuuza vyakula kama mayai na smokie.

• “Sakaja pia anafaa kuwalenga wasukuma na waendesha bodaboda... Nairobi ni jiji la biashara kubwa ya mamilioni,” aliongeza.

Mchuuzi wa mayai na kachumbari ahesabu hasara Kanju wakivamia.
Mchuuzi wa mayai na kachumbari ahesabu hasara Kanju wakivamia.
Image: Facebook

Mwanablogu mmoja kwenye mtandao wa Facebook, Councillor Njohi ameibua dhana tofauti kuhusu mjadala unaoendelea mitandaoni wa askari wa kaunti maarufu kanjo kuwahangaisha wachuuzi wa vyakula vidogo vidogo.

Wakati wengi wameonekana kuwakosoa vikali kanjo kwa kitendo cha Jumatano cha kumhangaisha mrembo mmoja mchuuzi wa mayai, kachumbari na smokie jijini kwa kutawanya mtaji wake na kutupa toroli lake kwenye gari lao, Njohi amewatete vikali kanjo na uongozi wa gavana Sakaja.

Kwa mujibu wa Njohi, jiji la Nairobi ni la wafanyibiashara wa mabilioni ya mtaji wala si jiji la kufanya biashara za kuchuuza vyakula kama mayai na smokie.

Njohi alisema kwamba jiji la Nairobi linalenga kuwa kama jiji la Dubai katika miaka michache ijayo na ili kufanikisha ndoto hiyo, ni lazima watu wa biashara za aibu kama hao wafukuzwe kabisa kutoka jijini ili kutoa nafasi kwa wawekezaji wenye mamilioni ya mitaji.

“Nairobi inatamani kuwa Dubai ijayo na unaweza kuona aina ya uwekezaji unaofanyika Eastleigh.... Maono hayo hayana nafasi kwa wachuuzi wa vyakula vya mitaani wasio na usafi wanaouza soseji na mayai ya kuchemsha kwa toroli, ambao hata hawalipi kodi za kaunti na ushuru. Asante Sakaja kwa kuwafukuza hao macho nje ya mji,” Njohi alisema.

Mwanablogu huyo pia alimsihi gavana Sakaja kuangazia katika sekta zingine za kusafisha jiji ikiwemo kuwafukuza waendesha bodaboda na wasukuma mikokoteni kutoka jijini.

“Sakaja pia anafaa kuwalenga wasukuma na waendesha bodaboda... Nairobi ni jiji la biashara kubwa ya mamilioni,” aliongeza.

Ukatili wa kanjo.
Ukatili wa kanjo.

Wakati hayo yanajiri, mwanaharakati Eric Omondi aliongoza wanamitandao kumchangishia mrembo aliyeathirika katika uvamizi huo wa kanjo.

Omondi alichangisha Zaidi ya nusu milioni ndani ya masaa 3 ya kwenda live na msichana huyo kwa jina Quinter Adhiambo ambaye mtaji wake wote ulitawanywa na kuharibiwa na Kanjo baada ya kupatikana akichuuza smokie na mayai kwa toroli lake katikati mwa jiji la Nairobi.