Raila apongeza watu wa Bomet kumfokea waziri Chirchir mbele ya rais Ruto wikendi

" Hata Bwana Ruto walimpatia tu heshima lakini hawakukubaliana na yale aliyokuwa akisema. Unajua anasema uongo." Raila alisema.

Muhtasari

• Watu walionesha ishara ya kukerwa na zogo ambalo linaendelea nchini la kumhusisha mfanyibiashara Anne Njeri.

Waziri wa kawi Davis Chirchir
DAVIS CHIRCHIR Waziri wa kawi Davis Chirchir
Image: EZEKIEL AMING'A

Kiongozi wa upinzani Raila Odinga ametoa pongezi na shukrani za dhati kwa wakaazi wa kaunti ya Bomet kwa kitendo cha kumfokea na kumzomea vikali waziri wa kawi, Davis Chirchir wikendi iliyopita.

Wikendi iliyopita, rais Ruto na viongozi mbali mbali wakiwemo baadhi ya mawaziri wake walihudhuria ibada ya kanisa katika kaunti ya Bomet ambapo baada ya ibada waliamua kuwahutubia wananchi.

Wakati waziri Chirchir anawahutubia watu, walionekana kuchukizwa na hotuba yake na kumzomea vikali mbele ya bosi wake – rais Ruto.

Ni kitendo ambacho kiliwakera wengi lakini kwa upande wa upinzani, kitendo hicho kinastahili.

“Bwana Chirchir, na mimi nataka kutoa shukrani kwa watu wa Bomet kwa kumuonesha adabu. Ndio ajue adabu na kuwa Wakenya wana shida. Hata Bwana Ruto walimpatia tu heshima lakini hawakukubaliana na yale aliyokuwa akisema. Unajua anasema uongo. Haitakikani mtu ambaye ni rais awe akisimama tu hivi anasema uongo, sema ukweli!” Raila alisema katika mkutano na vyombo vya habari wa muungano wa Azimio.

Watu walionesha ishara ya kukerwa na zogo ambalo linaendelea nchini la kumhusisha mfanyibiashara Anne Njeri anayedai kuwa shehena ya dizeli yenye thamani ya shilingi bilioni 17 ambayo imeshikiliwa katika bandari ya Mombasa kwa Zaidi ya mwezi ni yake.

Sakata hilo limekuwa likivutia pande mbalimbali, baadhi ya watu kutoka mrengo wa upinzani wakidai kwamba kuna watu ndani ya serikali wenye ushawishi mkubwa ambao wanamtumia Anne Njeri kuingiza mafuta hayo katika soko la humu nchini, Odinga kwa wakati mmoja akisema kwamba Njeri haonekani kuwa mtu mweney utajiri wa kiasi hicho.