UDA wageuza kibao sakata la dizeli ya 17b na kudai mafuta hayo ni ya Uhuru na Raila

"Tayari tunajua njama yenu katika sakata hili...Uhuru na Raila ni sharti waweke wazi msimamo wao katika sakata hili."

Muhtasari

• "Na mnaona vile haya mambo yametokea ndio Raila anaanza kuongea mambo ya mafuta. Uhuru Kenyatta pia ameamka." Malala alisema.

Katibu mkuu wa UDA Cleophas Malala
Katibu mkuu wa UDA Cleophas Malala
Image: Facebook

Utata kuhusu mmiliki halali wa shehena ya mafuta ya dizeli ya thamani ya shilingi bilioni 17 ambayo imekuwa ikishikiliwa katika bandari ya Mombasa kwa Zaidi ya mwezi unazidi kuibua mikondo tofauti.

Hii ni baada ya katibu mkuu wa chama tawala cha UDA, Cleophas Malala kuibua madai mengine mapya ya kuwahusisha rais mstaafu Uhuru Kenyatta na kinara wa ODM, Raila Odinga na shehe na hiyo ya dizeli.

Malala katika taarifa yake anadai kwamba wawili hao waliokuwa katika serikali ya Handshake wanamtumia mfanyibiashara Ann Njeri ili kufanikisha ajenda yao ya kuingiza mafuta hayo katika soko la Kenya.

Akihutubia wanahabari siku ya Jumanne, Malala alihoji ni kwa nini viongozi hao wawili wametoa maoni yao hadharani kuhusu hatua ya serikali ya kutaifisha shehena hiyo ya mafuta, huku akidokeza zaidi kwamba wawili hao wana maslahi katika usafirishaji huo.

"Hiyo yote ni propaganda ya kujaribu kuharibia serikali jina letu. Swali tunafaa kuuliza Njeri, biashara yake ya Kenya iko wapi chombo na akatengeneza Ksh.17 bilioni?" Malala alisema..

"Huyo mama hata kiosk hana na ako na Ksh.17 billion? Na mnaona vile haya mambo yametokea ndio Raila anaanza kuongea mambo ya mafuta. Uhuru Kenyatta pia ameamka."

Malala pia alidai kuwa pesa zilizotumika kununua mafuta ziliibwa kutoka kwa hazina ya umma wakati wa muhula wa mwisho wa Uhuru.

"Wakati tulienda kura mliskia kuna Ksh.16.9 bilioni ilipotea. Hiyo pesa walitoa kwa madola wakapeleka kwa makampuni yao kule nje. Sasa wameenda wakachukua pesa kule nje wakanunua mafuta ije kwa jina la Njeri hiyo ndio pesa irudi hapa Kenya," alisema.

"Tayari tunajua njama yenu katika sakata hili. Wameanza kutisha rais ndiyo rais akubali mafuta yao yaingie, hayo mafuta yakiingia wagawane pesa zao zile ambazo walikuwa wamepora Kenya. Uhuru na Raila ni sharti waweke wazi msimamo wao katika sakata hili."

Hayo yakiendelea, mfanyibiashara Ann Njeri anatarajiwa kufika mbele ya kamati ya bunge leo hii Jumatano kujitetea na kutoa uthibitisho kamili unaoonesha kwamba shehena hiyo ni yake kweli.