Rais Ruto amvika Faith Kipyegon taji la juu zaidi la kiheshima kwa raia, EGH

“Leo nimemvika mwanariadha wetu mshindi wa mbio za dunia, Faith Kipyegon, tuzo ya EGH, heshima ya juu Zaidi ambayo nchi yetu inawapa wananchi wake ambao wanaonesha picha halisi ya ubora." Ruto alisema.

Muhtasari

• "Pia ninawapongeza Ferdinand Omanyala, Mary Moraa, Kelvin Kiptum, Emmanuel Wanyonyi, Faith Cherotich ambao pia wamesajili matokeo ya kufurahisha" alisema.

MWANARIADHA FAITH KIPYEGON NA RAIS WILIAM RUTO
Image: TWITTER

Rais William Ruto amethibitisha kumvika mwanariadha mshikilizi mara mbili wa rekodi za dunia Faith Kipyegon kwa tuzo ya juu Zaidi ya Elder of the Order of the Golden Heart of Kenya (E.G.H.).

Kuvikwa huku kunajiri saa chache tu baada ya Kipyegon kushinda tuzo ya mwanariadha bora wa kike kote duniani katika hafla iliyofanyika usiku wa leo ya bodi ya riadha duniani.

Rais Ruto alithibitisha hili wakati wa hotuba yake ya sherehe za kuadhimisha miaka 60 ya uhuru wa Kenya, sikukuu ya Jamhuri katika uwanja wa Uhuru Gardens jijini Nairobi, Jumanne Desemba 12.

“Leo nimemvika mwanariadha wetu mshindi wa mbio za dunia, Faith Kipyegon, tuzo ya EGH, heshima ya juu Zaidi ambayo nchi yetu inawapa wananchi wake ambao wanaonesha picha halisi ya ubora. Yeye [Kipyegon] amejishindia nafasi yake katika ngazi za juu Zaidi, kutoka kukimbia miguu peku hadi kuvunja rekodi mbili za dunia ndani ya mwaka mmoja, ni ishara halisi ya ushujaa,” rais alisema.

Kiongozi huyo wa taifa pia alimsifia Kipyegon akisema kwamab safari yake ya mafanikio ni kichocheo safi kwa wanariadha chipukizi lakini pia akawapongeza wanariadha wengine ambao wamekuwa wakiipeperusha bendera ya Kenya katika michezo mbalimbali mwaka huu.

“Safari ya Faith ni kielelezo bora kwa wanariadha wachanga na wanaochipukia. Pia ninawapongeza Ferdinand Omanyala, Mary Moraa, Kelvin Kiptum, Emmanuel Wanyonyi, Faith Cherotich ambao pia wamesajili matokeo ya kufurahisha katika ulingo wa dunia, na wao pia watakuja kutuzwa tuzo za heshima,” Ruto alisema.

Order of the Golden Heart of Kenya ndio kitengo cha juu zaidi cha tuzo za urais ambacho kimegawanywa zaidi katika madaraja matatu: Chief of the Order of the Golden Heart of Kenya (C.G.H.), Elder of the Order of the Golden Heart of Kenya (E.G.H.) na Moran of the Order of the Golden Heart of Kenya (M.G.H.)

Elder of the Order of the Golden Heart of Kenya (E.G.H.) mara nyingi hupewa Naibu Rais, Maspika wa Bunge, Makatibu wa Baraza la Mawaziri, Mke wa Naibu Rais, Mkuu wa Utumishi wa Umma na Ulinzi wa Kenya na Mkuu wa Majeshi' (KDF).