KWS watoa njia 7 za kuepuka kushambuliwa na fisi, "Usitoroke, simama na uongee na fisi"

"Kupiga kelele kwa nguvu kunazua usumbufu kwake na atadhani unataka kumshambulia,” KWS waliongeza.

Muhtasari

• Kwa mujibu wa KWS, mtu hafai kukimbia pindi anapomuona fisi, kwani kukimbia ni sawa na kumchochea mnyama huyo mla mizoga kutaka kukufuata mbio.

• Idara hiyo pia iliwataka wananchi kutoonyesha woga wa aina yoyote pindi wanapokutana na fisi.

• KWS ilisema kwamba unafaa kusimama tisti na hata ikiwezekana uzungumze na mnyama huyo.

FISI
FISI
Image: HISANI

Shirika la wanyamapori nchini, KWS limetoa taratibu 7 za jinsi ya kuepuka kushambuliwa na fisi.

Hii ni baada ya visa vya fisi kuwashambulia wananchi vimeripotiwa kwa wingi katika siku za hivi majuzi haswa katika kaunti ya Kiambu.

Kupitia kurasa zao za mitandaono, KWS walitoa njia 7 za muhimu za kuhakikisha kwamba mtu unaepuka kushambuliwa na fisi, endapo utakutana nao njiani.

Kwa mujibu wa KWS, mtu hafai kukimbia pindi anapomuona fisi, kwani kukimbia ni sawa na kumchochea mnyama huyo mla mizoga kutaka kukufuata mbio.

KWS pia wanahoji kwamba mtu hafai kulala chali sakafuni kwa kuigiza kwamba amefariki kwani kufanya hivyo kunamsogeza karibu Zaidi fisi kutaka kunusa na hata kukupararua kwa meno kali.

Idara hiyo pia iliwataka wananchi kutoonyesha woga wa aina yoyote pindi wanapokutana na fisi.

KWS ilisema kwamba unafaa kusimama tisti na hata ikiwezekana uzungumze na mnyama huyo.

“Fisi haswa huwa ni wanyama wa usiku, kwa hivyo punguzeni kabisa kutembea nje usiku. Ukikutana na fisi, usiangalia upande mwingine hadi pale fisi mwenyewe atageuka, na hata hivyo, salia katika upande wa kumuangalia,” KWS ilisema kwa sehemu.

“Kama utamsikia fisi akibweka, usitoroke, simama imara, usitoroke lakini pia usimsogelee karibu. Kupiga kelele kwa nguvu kunazua usumbufu kwake na atadhani unataka kumshambulia,” KWS waliongeza.