Kiambu: Mrembo wa miaka 20 aliyetoweka kwa wiki 2 mwili wake wapatikana msituni

Polisi walifichua kuwa mwili wa mwanamke huyo ulipatikana ukiwa umetelekezwa msituni, ukiwa umetapakaa damu, na ukiwa na majeraha ambayo yaliashiria kuwa alinajisiwa.

Muhtasari

• Hiki ni takribani kisa cha 6 sasa kuripotiwa cha mauaji ya mwanamke katika mazingira tata humu nchini tangu mwaka 2024 ulipoanza.

Mwili wa marehemu
Mwili wa marehemu
Image: Instagram//Azam

Huku visa vya mauaji ya wanawake vikizidi kukithiri lakini pia kukemewa vikali na makundi mbalimbali humu nchini, polisi katika eneo la Lari Kaunti ya Kiambu wameupata mwili wa msichana wa miaka 20 aliyeripotiwa kutoweka takribani wiki mbili zilizopita.

Kwa mujibu wa Citizen, polisi wamelazimika kuanzisha uchunguzi  wakisema kwamba msichana huyo aliripotiwa kutoweka wiki mbili zilizopita kutoka kijijini kwao Kinare kabla ya mwili wake kupatikana ukiwa umetupwa katika msitu wa Kinare.

Polisi walifichua kuwa mwili wa mwanamke huyo ulipatikana ukiwa umetelekezwa msituni, ukiwa umetapakaa damu, na ukiwa na majeraha ambayo yaliashiria kuwa alinajisiwa.

Mwili wake ulihamishwa hadi katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Wilaya ya Naivasha, ukisubiri uchunguzi wa maiti. Wakaazi wa eneo hilo wamelalamikia msitu huo wakisema kuwa umegeuka kuwa mahali pa kufanyia uhalifu kama vile mauaji wakirejelea visa kadhaa vilivyoshuhudiwa katika msitu huo.

Hiki ni takribani kisa cha 6 sasa kuripotiwa cha mauaji ya mwanamke katika mazingira tata humu nchini tangu mwaka 2024 ulipoanza.

Wikendi iliyopita, kundi la wanawake jijini Nairobi liliandaa maandamano ya Amani jijini Nairobi wakiteta vikali dhidi ya mauaji hayo ambayo wanahisi yanawalenga watu wa jinsia ya kike.

Kundi hilo liliongozwa na mwakilishi wa wanawake kaunti ya Nairobi, Esther Passaris na ujumbe wa wito wao ulikuwa kuwataka wanaume kukoma kuwaua watu wa jinsi ya kike.