DCI wafichua sura ya mshukiwa mkuu wa mauaji ya Rita Waeni, waomba kusaidiwa kumpata

Idara hiyo imetoa wito kwa wananchi kutoa taarifa zitakazofanikisha kukamatwa kwa mshukiwa mkuu.

Muhtasari

•Katika taarifa Jumatano, idara hiyo ilifichua kuwa maafisa wake sasa wako katika hatua ya juu ya uchunguzi wa mauaji ya binti huyo wa miaka 20

•Walichapisha  picha za CCTV za mshukiwa mkuu na kumtaka yeyote aliye na habari kuhusu mwanaume huyo kuzishiriki na mamlaka.

DCI wameomba usaidizi wa kumpata mshukiwa mkuu wa mauaji ya Rita Waeni
Image: HISANI// DCI

Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) imetoa taarifa kuhusu maendeleo ya uchunguzi wa mauaji ya kutisha ya Rita Waeni yaliyotokea mapema mwaka huu.

Katika taarifa Jumatano, idara hiyo ilifichua kuwa maafisa wake sasa wako katika hatua ya juu ya uchunguzi wa mauaji ya binti huyo wa miaka 20

Walifichua kuwa uchunguzi wa kina umefanywa kubaini dakika za mwisho za marehemu  na mshukiwa mkuu wa mauaji yake, ambaye bado hajakamatwa. 

"Zaidi, taarifa za kina za watu wanahusishwa zimerekodiwa na data zaidi kutoka kwa mifumo ya kidijitali ili kuhakikisha kwamba vidokezo vyote vya wauaji wa Rita vimetumika.

Kwa bahati mbaya, mshukiwa mkuu wa mauaji hayo, mwanamume aliyenaswa pekee na kamera za CCTV akimtembeza Rita hadi kwenye eneo la kifo chake amesalia mitini, na timu ya Uchunguzi wa Mauaji ya DCI haina rasilimali katika harakati zake,” DCI ilisema kwenye taarifa yake kwenye mtandao wa Twitter.

Baada ya kutofanikiwa kumpata mshukiwa mkuu wa mauaji hayo ya kinyama, sasa makachero wametoa wito kwa wananchi kutoa taarifa zitakazofanikisha kukamatwa kwake.

Walichapisha  picha za CCTV za mshukiwa mkuu na kumtaka yeyote aliye na habari kuhusu mwanaume huyo kuzishiriki na mamlaka.

"Ingawa utambulisho wake bado haujajulikana, imethibitishwa kuwa alianza mawasiliano na marehemu Waeni mnamo Oktoba 2, 2023 kupitia akaunti ya Instagram kwa majina ya Carlton Maina (pseudo), jina ambalo lilibadilishwa mara kadhaa na hatimaye kuvutwa. chini mara baada ya mauaji ya kinyama.

Mshukiwa huyo anaaminika kuzuru hoteli kadhaa Nairobi Magharibi mnamo Oktoba 2023 na Green House Airbnb iliyoko Roysambu kando ya TRM Drive mnamo Nov 7 na Nov 11, 2023.

Anaaminika pia kuwa na akili ya uhalifu inayothibitishwa na njia yake ya kukwepa kamera za CCTV. Anafahamu Kiswahili na Kiingereza vizuri, na ana ujuzi wa Nairobi na viunga vyake,” DCI ilisema.

Ili kushiriki habari zozote kuhusu utambulisho wa mshukiwa au mahali alipo, DCI imewataka wananchi kuwapigia simu kupitia nambari ya simu ya bure 0800 722 203, au kuripoti kwa kituo chochote cha polisi au afisa wa polisi.