Waandamanaji wafika kwenye afisi ya mbunge wa Nyali Mohammed Ali

Kundi hilo lilitaka kujua msimamo wa Mohammed Ali kwenye mswada wa fedha 2024

Muhtasari

•Mbunge huyo hakuwepo katika bunge la kitaifa wakati wenzake walipokuwa wakipigia kura mswada wa fedha wa 2024.

• Kikundi cha vijana kiliandamana hadi afisi yake Nyali ambapo walitafuta majibu yake ikiwa anaunga mkono mswada wa fedha au la.

Kundi la vijana wakiwa nje ya lango kuu la afisi ya mbunge wa Nyali,Mohammed Ali
Kundi la vijana wakiwa nje ya lango kuu la afisi ya mbunge wa Nyali,Mohammed Ali
Image: Aura Ruth

Kundi la waandamanaji wanaopinga mswada wa fedha  walitinga kwenye  afisi ya mbunge wa Nyali Mohamed Ali  kwa madai ya mbunge huyo kushindwa kutangaza msimamo kuhusu mswada wa fedha wa 2024.

Mbunge huyo hakuwepo katika bunge la kitaifa wakati wenzake walipokuwa wakipigia kura mswada wa fedha wa 2024. Kikundi cha vijana kiliandamana hadi afisi yake kule Nyali.Vijana hao walitaka majibu yake ikiwa anaunga mkono mswada wa fedha au la.

Lydia Adhiambo,mmoja wa vijana alisema wana wasiwasi kuwa mbunge huyo hajaweka wazi msimamo wake kuhusu suala hilo.

"Hii leo ikiwa ni Jumatatu, ujumbe wetu ni kwamba mamlaka ni ya watu. Kura yetu ndiyo iliyomfikisha hapo alipo. Tulikuja kumsalimia na kumjulisha kuwa tunamtazama..." Lydia  alisema.

Aliongeza ,"Ni sharti kwa  mbunge Ali kukataa  mswada wa fedha hana jawabu lingine wala  hakuna kingine."

Wakati wa maandamano ya kupinga mapenzi ya jinsia moja [LGBTQ] Adhiambo alimpongeza mbunge huyo kwa kujitokeza kuwaunga mkono.

Vijana hao walimtaka mbunge huyo pia kusimama nao kwenye suala la mswada wa fedha 2024.

Tutakuletea taarifa zaidi.