Uhuru Kenyatta atoa wito kwa viongozi kuwasikiliza wananchi maandamano yakigeuka vurugu

Katika taarifa yake, Uhuru aliwashauri viongozi waliochaguliwa kukumbatia mazungumzo na kutafuta suluhu kwa masuala yanayowakabili Wakenya.

Muhtasari

• Kulingana na Uhuru, kusikiliza halikuwa chaguo la viongozi waliochaguliwa bali ni agizo.

• Rais huyo wa zamani pia alielezea masikitiko yake kuhusu kupoteza maisha ambayo yalishuhudiwa katika maandamano ya Jumanne.

Rais mstaafu Uhuru Kenyatta
Rais mstaafu Uhuru Kenyatta
Image: Hisani

Rais wa zamani Uhuru Kenyatta ameitaka serikali kuwasikiliza Wakenya kufuatia maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha ambayo yalizua taharuki siku ya Jumanne, Juni 25.

Katika taarifa yake, Uhuru aliwashauri viongozi waliochaguliwa kukumbatia mazungumzo na kutafuta suluhu kwa masuala yanayowakabili Wakenya.

Kulingana na Uhuru, kusikiliza halikuwa chaguo la viongozi waliochaguliwa bali ni agizo.

Rais huyo wa zamani pia alielezea masikitiko yake kuhusu kupoteza maisha ambayo yalishuhudiwa katika maandamano ya Jumanne.

"Wakati huu wa majaribu kwa Nchi yetu, nataka kuwakumbusha viongozi wote kwamba walichaguliwa na wananchi.”

"Kuwasikiliza watu sio chaguo bali ni jukumu lililowekwa katika misingi ya katiba yetu na katika misingi na falsafa ya demokrasia," alisema.

Uhuru aliyasema hayo punde tu baada ya rais William Ruto kuhutubia taifa. Katika hotuba yake, Ruto alielezea matukio ya Jumanne kama ya uhaini.

Ruto alidai kuwa maandamano hayo ya amani yametekwa nyara na wahalifu na kuongeza kuwa serikali itapinga vitendo vyao.

"Nimeagiza vyombo vyote vya usalama wa taifa kupeleka hatua za kuzuia majaribio yoyote ya wahalifu hatari kuhujumu usalama na uthabiti wa nchi yetu," Ruto alisema.

"Wananchi wa Kenya wanakwenda kulala usiku wa leo, ninawapa hakikisho langu kwamba usalama wa familia na mali zenu unasalia kuwa kipaumbele changu kikuu."