Rais Ruto kuzungumza na vijana kwenye X -Space, saa 8 alasiri

Mazungumzo hayo yanaratibiwa kuanza saa nane mchana hadi saa kumi na moja jioni leo.

Muhtasari

•Wakenya wamealikwa kujiunga na mjadala wa X Space kuanzia saa nane mchana hadi saa kumi na moja jioni.

•"Nataka tujadili kuhusu kodi, nataka tujadili ukosefu wa ajira, ufisadi, masuala yote,” Rais alisema wakati wa mahojiano na waandishi wa habari kule  Ikulu Juni 30.

Rais Ruto
Image: twitter

Rais William Ruto anatazamiwa  kuwa mwenyeji wa mazungumzo yake ya kwanza ya X-Space (zamani Twitter) na vijana wa Kenya mwendo wa saa nane mchana hadi saa kumi na moja jioni leo.

Kulingana na Ikulu, baraza la mawaziri limepangwa kujiunga na majadiliano ya mtandaoni ya saa tatu. 'X Spaces', ni kipengele kinachokuruhusu kuwa na mazungumzo ya moja kwa moja ya sauti kwenye jukwaa la mitandao ya kijamii.

Tangazo hilo lilitolewa katika vyombo vya habari baada ya kikao cha baraza la mawaziri kilichoongozwa na rais kwenye  Ikulu ,Alhamisi Julai 5 ,2024.

Wakenya wamealikwa kujiunga na mjadala wa X Space kuanzia saa nane mchana hadi saa kumi na moja jioni.

"Wakenya wote wanakaribishwa kuchangia mazungumzo haya kama sehemu ya juhudi zetu za pamoja za kukuza upya wa kitaifa na kuunda Kenya bora kwa wote," 

Maendeleo hayo yanakuja kufuatia maandamano ya Gen Zs kushinikiza mageuzi ya utawala. Maandamano ya awali ya kitaifa dhidi ya mswada wa fedha wa 2024 ambao umetupiliwa mbali, yalishuhudia maelfu ya vijana wa Kenya wakiingia mitaani kwa wiki mbili.

Katika mahojiano ya pamoja ya wanahabari kwenye televisheni hapo awali, mkuu wa nchi alisema yuko tayari kuwashirikisha vijana kwenye jukwaa analopenda.

"Ninasikia kwamba vijana wanasema hatutaki jukwaa la sekta nyingi, labda tuwe na mazungumzo  na Rais kwenye X. Niko wazi kwa mazungumzo na vijana kwenye jukwaa ambalo wanafurahi. Wakitaka nishirikiane nao kwenye X, nitakuwepo. Nataka tujadili kuhusu kodi, nataka tujadili ukosefu wa ajira, ufisadi, masuala yote,” alisema wakati wa mahojiano na waandishi wa habari kule  Ikulu.