"Naumia!" Msanii Kareh B alilia majibu kufuatia kifo cha mwanawe katika ajali ya Chavakali, alalamikia serikali

“Serikali, mna maoni gani katika suala hili? Je, mtaendelea kuwa kimya na kupoteza watoto wengi zaidi barabarani?" Kareh B alilalamika.

Muhtasari

•Kareh B sasa ametaka majibu kuhusu kifo cha mwanawe, akifichua kuwa hayuko sawa kufuatia tukio hilo la kusikitisha.

•Ametaka serikali kutoa majibu kuhusiana na ajali za barabarani, suala ambalo amewataka kushughulikia kwa dharura.

alimpoteza mwanawe Joseph Maduli mnamo Aprili 1, 2024.
Msanii Kareh B alimpoteza mwanawe Joseph Maduli mnamo Aprili 1, 2024.
Image: HISANI

Mwimbaji maarufu wa Mugithi Mary Wangary Gioche almaarufu Kareh B ameendelea kuomboleza kufuatia kifo cha mwanawe wa miaka 17, Joseph Maduli, aliyefariki katika ajali ya basi la Easy Coach iliyotokea eneo la Mamboleo, kaunti ya Kisumu mnamo Aprili 1, 2024.

Joseph ambaye alikuwa mwanafunzi wa kidato cha nne katika Shule ya Upili ya Wavulana ya Chavakali alifariki siku ya Jumatatu usiku baada ya basi walimokuwa wamepanda kuwapeleka nyumbani kwa likizo ya Aprili kuanguka katika makutano ya Mamboleo.

Akizungumza kupitia kurasa zake za mitandao yake ya kijamii, Kareh B sasa ametaka majibu kuhusu kifo cha mwanawe, akifichua kuwa hayuko sawa kufuatia tukio hilo la kusikitisha.

"Nahitaji majibu, navunjika," Kareh B alisema kupitia Facebook.

Alidai kuwa bado hajapata taarifa kuhusu kifo cha mtoto wake na kile kilichotokea. Pia alilalamikia suala la watoto wa shule kusafiri usiku.

Msanii huyo kutoka kaunti ya Murang’a pia aliitaka serikali kutoa majibu kuhusiana na ajali za barabarani, suala ambalo amewataka kushughulikia kwa dharura.

“Serikali; mna maoni gani katika Suala hili? Je, mtaendelea kuwa kimya na kupoteza watoto wengi zaidi barabarani?

Je, ni hatua gani unaweka ili kupunguza ajali zinazotokea nchini hasa vijana wa kizazi kipya? Je, tunahitaji kumfufua Michuki?” Aliandika.

Aliongeza, “Nahitaji Majibu. Nenda sawa mwanangu."

Kareh B alizungumza na Citizen TV siku ya Jumanne ambapo alieleza jinsi alivyopata habari kuhusu ajali hiyo kupitia mitandao ya kijamii usiku wa kuamkia Jumanne. Alisema kuwa yeye pamoja na wazazi wengine  tayari walikuwa wameeleza wasiwasi wao kuhusu wanafunzi hao kusafiri usiku, lakini ndio ulikuwa mpango pekee wa safari ambao shule iliweza kuwaandalia wanafunzi hao.

“Sikupata usingizi. Mwendo wa kati ya saa sita unusu na saa saba usiku, habari kwenye mitandao ya kijamii. Hapo ndo nilipata ujumbe kwamba basi ambayo imeanguka ya Chavakali,” alisema Kareh B.

Mwimbaji huyo alisema alikuja kujua kwamba mwanawe alifariki katika ajali hiyo siku ya Jumanne asubuhi, saa kadhaa baada ya ajali hiyo kutokea.

Alibaini kuwa mwanawe aliaga baada ya wanafunzi wengi waliosafiri kutoka Kisumu hadi Nairobi kufika Nairobi Jumanne asubuhi, lakini mwanawe akakosa kufika.

“Nilianza kujiuliza mbona wangu hajafika. Nikiuliza mmoja wa waalimu ambaye alisema alikuwa kwenye eneo la ajali, ananiambia wale ambao walipata majeraha kidogo walipewa ruhusa ya kupigia wazazi wao wawaambie usiwe na wasiwasi niko hospitalini niko sawa,” alisema