Muthoni afichua sababu ya kumtaka Mama Ngina anyoe nywele zake

Muhtasari
  • Mpigania uhuru huyo alishughulikia masuala hayo siku nne baada ya hafla hiyo ya Jumamosi
  • Muthoni alisema aliamua kunyoa nywele zake ili kuashiria kuwa Kenya imepata uhuru kamili
Image: Hisani

Field Marshal Muthoni Wa Kirima amefafanua ni kwa nini alimruhusu aliyekuwa Mama Rais Mama Ngina Kenyatta kunyoa dreadlocks zake.

Baada ya kuvuga nywele hizo kwa zaidi ya miaka 70, kama ushuhuda wa kupigania uhuru, Muthoni alizikata Jumamosi, Aprili 2.

Mama Ngina aliongoza sherehe hizo, huku wawili hao wakikumbuka maisha yao ya ujana, urafiki na kupigania uhuru.

Akithibitisha hatua ya kunyoa nywele zake zenye urefu wa futi sita, Muthoni alipuuzilia mbali ripoti zinazodai kuwa Mama Ngina alimlazimisha kunyoa.

Mpigania uhuru huyo alishughulikia masuala hayo siku nne baada ya hafla hiyo ya Jumamosi.

Muthoni alisema aliamua kunyoa nywele zake ili kuashiria kuwa Kenya imepata uhuru kamili.

"Nililazimika kuzikata kwa sababu imekuwa safari ndefu. Nilianza kutunza nywele hizi mwaka wa 1952 na baada ya zaidi ya miaka 70, nilihitaji kuziondoa. Sasa ninahisi kama msichana mdogo," Muthoni alisema.

"Hakuna mtu anayeweza kunyoa nywele zangu bila idhini yangu. Kama wangejaribu kufanya hivyo, ningewapiga vizuri," aliongeza.

Mama Ngina Kenyatta aliongoza hafla maalum ya kunyoa dreadlocks za Field Marshal  katika Mji wa Nyeri mnamo Jumamosi.

Mpiganaji huyo wa Mau Mau amekuwa na dreadlocks kwa zaidi ya miaka 70.

Wengi wa wapiganaji wa Mau Mau waliapa kwamba hawatawahi kunyoa hadi wazungu waondoke Kenya.

Tamaa ya mkongwe huyo ilikuwa kumtaka Mama Ngina kukata dreadlocks zake na kumbariki Rais Uhuru Kenyatta.