Boniface Mwangi azungumza baada ya kuhusika katika ajali, kusababisha uharibifu hospitalini

Mwanaharakati huyo amesema baada ya ajali mkewe alikuwa akiumwa na katika hali ya kuchanganyikiwa.

Muhtasari

•Mwangi alisema ajali hiyo ilitokea katika barabara ya Lang'ata mnamo Agosti 21 baada ya dereva aliyekuwa akiendesha gari kwa kasi kujipenyeza kwenye njia yao na kuligonga gari lao.

•Baba huyo wa watoto watatu alisema wakati walipofika hospitalini mkewe alikuwa akiumwa na katika hali ya kuchanganyikiwa.

Image: FACEBOOK// BONIFACE MWANGI

Mwanaharakati mashuhuri Boniface Mwangi amefichua kuwa alihusika kwenye ajali ya barabarani siku kadhaa zilizopita.

Katika taarifa aliyotoa Alhamisi, Mwangi alisema ajali hiyo ilitokea katika barabara ya Lang'ata mnamo Agosti 21 baada ya dereva aliyekuwa akiendesha gari kwa kasi kujipenyeza kwenye njia yao na kuligonga gari lao.

Mwanaharakati huyo alisema baada ya gari lao kugongwa lilipinduka na kutua juu chini.

"Tulitua juu chini na watu wa kwanza kufika kwenye eneo la tukio walitupora vitu zetu za kibinafsi. Kwa bahati nzuri, wanandoa wasamaria wema, Eddu Rono na mke wake, Koskey Yuniscah, walikuja kutuokoa na kutupeleka hospitalini," Alisema.

Baba huyo wa watoto watatu alisema wakati walipofika hospitalini mkewe alikuwa akiumwa na katika hali ya kuchanganyikiwa.

Amedai kuwa aliagizwa kulipa kwanza ili mkewe aweze kuhudumiwa ila hakuwa na chochote mfukoni, jambo lililofanya azue vurugu pale hospitalini na baadae kukamatwa na kuzuiliwa katika kituo cha polisi.

"Mke wangu alipata matibabu aliyohitaji wakati rafiki yangu alipokuja hospitalini na kulipa bili. Mimi na familia yangu tunashukuru kwamba mke wangu hakupata majeraha mabaya. Uongozi wa hospitali hiyo uliita polisi ambao walinikamata. Nilifungwa katika Kituo cha Polisi cha Akila," Alisimulia mwanaharakati huyo.

Mwangi amesema baada ya kuachiliwa alirudi pale hospitalini na kuomba msamaha kwa uharibifu ambao alifanya.

Pia alilazimika kulipa Ksh 106,000 kufidia uharibifu aliosababisha katika eneo la mapokezi ya wageni ya hospitali hiyo.

"Wasiwasi wangu ni; kwa nini Wakenya wengi ambao huishia kuwa wa kwanza kwenye eneo la ajali huiba badala ya kusaidia? Kwa nini hospitali zinahitaji amana ili kusimamia matibabu ya dharura? Je, faida huleta maisha? Watu wengi sana wamekufa na wanaendelea kufia kwenye korido za hospitali kwa sababu madaktari hawatawagusa bila amana. Je, tunathamini faida kuliko maisha ya binadamu?" Mwangi alihoji.

Mwanaharakati huyo alilazimika kujitetea baada ya video iliyomuonyesha akizua vurugu hospitalini kusambaa kwenye mitandao ya kijamii.

Tetesi kwenye mitandao ya kijamii zilisema kwamba alikuwa amebugia kileo wakati aliposababisha drama zile.