Makamishna waliojitenga ndio walienda Ugiriki kuangalia uchapishaji - wakili Kamau Karori

Wakili Karori alikuwa akitetea IEBC na mwenyekiti wake Wafula Chebukati

Muhtasari

• Alitilia shaka kujitenga kwa mawakili wanne licha ya kwamab wao ndio waliwakilisha tume huko Ugiriki katika shughuli ya kuangalia uchapishaji wa karatasi za kupiga kura.

Mwanasheria Kamau Karori akiwakilisha IEBC
Mwanasheria Kamau Karori akiwakilisha IEBC
Image: Kenya judiciary//twitter

Wakili wa mwenyekiti wa tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC mwanasheria Kamau Karori amemtetea vikali Chebukati dhidi ya shtuma zilizotolewa na makamishne wanne waliojitenga na matokeo ya uchaguzi wa urais.

Katika utetezi wake, Karori alisema kauli ambayo ilionekana kuwiana na swali la jaji Lenaola aliyetilia shaka kujiondoa kwa makamishna hao kwa madai kwamab hawawezi kujihusisha na matokeo hayo licha ya kuonekana awali kuyatangaza huku shughuli ya kuhesabu kura ilipokuwa ikiendelea.

Karori alisema kwamba makamishna hao wanne waliojitenga na matokeo walisafiri mpaka nchini Ugiriki kukagua karatasi na vifaa vyote vya kuendesha shughuli ya uchaguzi.

Makamishna hao ndio waliwakilisha tume ya IEBC katika uangalizi wa shughuli ya uchapishaji wa karatasi za kupiga kura kulingana na Karori.

Kulingana na wasilisho la Karori katika kutetea tume ya IEBC na Mwenyekiti wake, makamishna wanne waasi hawana sababu yoyote ya kujitenga na uchaguzi pamoja na matokeo yote kwani walionekana hadharani wakishiriki katika mchakato wote usiku na mchana.

“Kabla ya karatasi za kupiga kura zisafirishwe nchini, makamishna ambao sasa ni walalamishi walikwenda nchini Ugiriki kufanya uangalizi jinsi uchapishaji ulivyokuwa ukiendelea. Wao ndio waliwakilisha tume ya IEBC huko,” Karori alisema.