Fred Ngatia, wakili wa Ruto aomba msamaha baada ya jaji kumpasha kwa kunong'ona kortini

“Ninaomba radhi kwa mheshimiwa jaji wa mahakama ya upeo" - Ngatia

Muhtasari

• “Wewe kama mshauri mkuu wa kisheria, unafaa kujua jinsi ya kujibeba ndani ya mahakama,” Jaji Wanjala alimwambia.

Mshauri mkuu wa kisheria Fred Ngatia
Mshauri mkuu wa kisheria Fred Ngatia
Image: Screenshot//Youtube

Huku matayarisho ya kusikilizwa kwa kesi iliyowasilishwa katika mahakama ya upeo kupinga matokeo ya urais yaliyotangazwa na tume ya IEBC kumpa Ruto ushindi, Jumanne kikao cha utangulizi wa kusikilizwa kwa kesi hiyo kilifanyika huku mawakili na wanasheria mbali mbali wakijitokeza kujitambulisha na upande watakaowakilisha kwenye kesi hiyo.

Katika tukio lisilo la kawaida, mshauri mkuu wa kisheria Fred Ngatia alionekana akinong’ona katika mahakama hiyo mbele ya jopo la majaji.

Jaji Smokin Wanjala alionekana kutolifurahia jambo hilo ambapo alimpasha Ngatia na kumtaka ajirekebishe kwani yeye kama mshauri wa kisheria wa muda mrefu anajua jinsi watu wanafaa kujibeba wakiwa katika mahakama yenye hadhi kama hiyo.

“Wewe kama mshauri mkuu wa kisheria, unafaa kujua jinsi ya kujibeba ndani ya mahakama,” Jaji Wanjala alimwambia.

Ngatia alilazimika kuomba radhi kutokana na kitendo cha kunong’ona mahakamani na kusema kwamba mnong’ono huo haukuwa wa mahakama bali ulikuwa tu kwa wakili mwenzake.

“Ninaomba radhi kwa mheshimiwa jaji wa mahakama ya upeo na ahsante kwa kunikumbusha tena. Mnong’ono haukuwa wa mahakama bali kwa wakili msomi mwenzangu,” Ngatia aliomba radhi.

Ukatizaji huo ulikuja muda mfupi baada ya Ngatia, mmoja wa mawakili wanaomwakilisha Rais Mteule William Ruto katika Mahakama ya Juu, kuhoji benchi inayoongozwa na Martha Koome kuhusu uamuzi wake wa kuweka kundi la mawakili wa DP kuwa wanne pekee.

Katika wasilisho lake katika Mahakama ya Juu Jumanne, Agosti 30, Ngatia aliteta kuwa agizo hilo lilikuwa la adhabu kwa Rais Mteule.

Aidha alilalamika kuwa walalamishi wengine wote waliruhusiwa kuwa na takriban mawakili 16 ilhali maombi yao yote yalilenga kubatilisha uchaguzi wa Ruto.

Wasilisho lake linajiri saa chache baada ya Mahakama ya Juu Zaidi kuamua kuwa Raila Odinga, William Ruto, na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) watawakilishwa na mawakili wanne kila mmoja.