Gladys Shollei - Orengo, mahakama ya upeo si baraza la chifu la kupelekewa porojo!

Hiyo kesi yenu hakuna mahali itaenda! - Shollei alimwambia Orengo

Muhtasari

• “Mahakama ya upeo si baraza la kupelea porojo. Ni sehemu ya kuenda kuchanganua uhalali wa matokeo ya urais" - Shollei.

• Kwa ujasiri mkubwa alisema kesi ya Azimio dhidi ya IEBC na Ruto hakuna mahali itaenda.

Mwakilishi wa kike wa Uasin Gishu amemkejeli gavana wa Siaya kwa kushiriki kuwasilisha ombi mahakamani kutaka kubatilisha ushindi wa Ruto.
James Orengo, Gladys Shollei Mwakilishi wa kike wa Uasin Gishu amemkejeli gavana wa Siaya kwa kushiriki kuwasilisha ombi mahakamani kutaka kubatilisha ushindi wa Ruto.
Image: Twitter

Mwakilishi wa kike katika kaunti ya Uasin Gishu Gladys Boss Shollei ambaye ni mtetezi mkali wa sera za naibu rais anayeondoka William Ruto amemjia juu vikali wakili na ambaye ni gavana mteule wa Siaya James Orengo kwa kile alisema kwamba ni aibu kwa wakili mwenye heshika kama huyo kuchukua kesi mahakamani akijua haitakuwa na tija.

Akizungumza katika hafla ya kuapishwa kwa Jonathan Chelilim almaarufu Koti Moja kama gavana wa pili wa kaunti hiyo ya bonde la ufa, Shollei alimzomea Orengo na kusema kwamba katika uwakili wake tayari amemshinda Orengo kwa sababu alifeli kwa kushiriki kuwasilishwa kwa ombi katika mahakama ya upeo ili kubatilisha ushindi wa rais mteule William Ruto.

“Na nawaeleza tafahdali rafiki zangu katika ule upande mwingine, nataka mwambie mawakili wenu, na Orengo tafadhali wewe ni mshauri wa kisheria mkubwa lakini sasa ni wazi kwamba mimi ni mshauri mkubwa kukuliko, kwa sababu inatokeaje kwamba hujui kuwa mahakama ya upeo si baraza la chifu?” Shollei aliuliza.

Shollei alizidi kumshambulia Orengo kwa kumpa funzo kidogo kuhusu maana halisi ya mahakama ya upeo huku akimwambia ile ni sehemu ya kupeleka maombi ya kesi maalumu zisizotaka mchezo kama kesi ya kutaka kubatilishwa kwa ushindi wa Ruto.

“Mahakama ya upeo si baraza la kupelea porojo. Ni sehemu ya kuenda kuchanganua uhalali wa matokeo ya urais. Kwa hiyo wacha kubeba kura ya maoni katika mahakama. Wacha kubeba fitina ya Githongo kuelekea mahakamani,” Shollei alitema cheche huku pia akikata nyembe ndani zaidi katika ombi la mpiga kura Githongo aliyedai ana Ushahidi wa video kuonesha jinsi kura zilivyoibwa kwa upendeleo wa Ruto.

Mwanamke huyo mwenye misimamo isiyotetereka dhidi ya wakosoaji wa Ruto aliwarai watu wa Uasin Gishu kuwa na utulivu huku akiwapa hakikisho kwamba kesi ya kutaka ushindi wa Ruto kubatilishwa haitaenda mahali na itasambaratika mbele ya mahakama ya upeo.

“Hiyo kesi hakuna mahali itaenda, kwa hiyo mtulie na mjue kila kitu kiko sawa,” Shollei alisema.