Tuju alitaka IEBC itangaza Odinga kuwa mshindi la sivyo uchaguzi urudiwe kwa lazima - Guliye

Cherera alitaka kutaka zaidi ya kura 230,000 kutoka kwa kapu la Ruto ili marudio ya kura yafanyike - Abdi Guliye.

Muhtasari

• “Badala yake, Tuju alipendekeza ikitokea haiwezekani kumtangaza ‘baba’ kuwa rais mteule, basi tume ilazimishe marudio ya uchaguzi," - Guliye.

Kamishna wa IEBC Abdi Guliye asema katibu wa Jubilee Raphael Tuju alitaka walazimishe marudio ya uchaguzi
Kamishna wa IEBC Abdi Guliye asema katibu wa Jubilee Raphael Tuju alitaka walazimishe marudio ya uchaguzi
Image: Maktaba, Twitter

Kamishna wa IEBC Abdi Guliye amewasilisha majibu yake kuhusu ombi la uchaguzi wa urais lililowasilishwa katika Mahakama ya upeo na muungano wa Azimio la Umoja One Kenya.

Katika kile ambacho sasa kinachukua mkondo tofauti kabisa usiotabirika na unaozidi kuwa changamano zaidi huku sasa mpira wa lawama ukirushwa kutoka sehemu moja ya meza kuelekea nyingine kama mpira wa kitenesi, Guliye amesema kwamba katibu mkuu wa chama cha Jubilee Raphael Tuju aliwafuata makamishna hao usiku wa manane akiwarai kumuidhinisha Raila kama mshindi huku akiwaahidi posho nene endapo wangefanikisha njama hiyo.

Katika hati yake ya kiapo, Guliye alidai kuwa makamu mwenyekiti wa tume hiyo Juliana Cherera alijaribu kushawishi matokeo ya kura ili kuandaa duru ya pili. Guliye alisema lengo la Cherera katika majaribio yake lilikuwa ni kutaka zaidi ya kura 230,000 kutoka kwa kapu la Ruto ili marudio ya kura yafanyike.

Kamishna huyo alisema baadhi ya viongozi kutoka muungano wa Azimio walikuwa wanawafuata usiku kuwarai huku kando na kumtaja Tuju pia alimtaja seneta wa Busia Amos Wako.

“Takriban saa tatu asubuhi ya Agosti 15, mwenyekiti alitembelewa na Raphael Tuju, seneta Amos Wako na Wakili Kyalo Mbob," Guliye alisema.

Katika hati hiyo ambayo Guliye aliiwasilisha mahakamani alasiri ya Jumamosi, alisema kwamba seneta Wako aliitaka IEBC kumtangaza Raila ili kudumisha amani na kusema kwamab waliambiwa ikiwa wataenda kinyume na takwa hilo basi taifa lingetumbukia kwenye mzozo.

“Wako alidokeza kuwa wamekuja kuitaka tume hiyo isifanye kazi ‘kwa ombwe’, na kwamba lazima izingatie uhusiano kati ya matokeo ya uchaguzi yatakayotangazwa na utulivu wa nchi, jambo ambalo alilitaja kuwa ‘picha kubwa’. Wako aliendelea kuashiria kuwa katika muhula wake kama Mwanasheria Mkuu, pia alihudumu kama msimamizi wa uchaguzi na katika wadhifa huo, angesawazisha matokeo kwa kuongozwa na hitaji la kufikia sheria na utulivu nchini," Guliye anasema kwenye hati hiyo ya kiapo.

Kamishna huyo alizidi kusema kwamba katibu mkuu wa Jubilee Tuju aliwataka walazimishe uchaguzi kurudiwa endapo ingekuwa vigumu kukoroga takwimu kwa upendeleo wa Odinga.

“Badala yake, alipendekeza ikitokea haiwezekani kumtangaza ‘baba’ kuwa rais mteule, basi tume ilazimishe marudio ya uchaguzi," sehemu ya kiapo hicho ilisoma.