Muonekano mpya! Sidika aibuka baada ya kufanya sajari ya makalio

Mwanasosholaiti Vera Sidika asema kuwa amefanyiwa upasuaji wa kupunguza makalio yake

Muhtasari

• Aliwashauri wanadada ambao wangetaka kufanyiwa upasuaji wa kimwili kuukubali mwili wao na kubaki walivyo kwani itawaletea shida huko mbeleni.

• Sidika aliwashukuru mashabiki wake kwa kumuunga mkono na kumwonyesha upendo na aliwahimiza wamsaidie ka safari hii yake mpya.

Image: VERA SIDIKA//INSTAGRAM

Mwanasosholaiti Vera Sidika asema kuwa amefanyiwa upasuaji wa kupunguza makalio yake na hata kuchapisha mtandaoni picha iliyoonyesha mabadiliko yake.

Sidika alisema kuwa ilibidi afanyiwe upasuaji huo kwa kuwa upasuaji wa kuubadilisha mwili wake umemletea shida baadaye ikiwemo shida ya kiafya.

Mama huyo wa mtoto mmoja aliongeza na kusema kuwa safari hiyo ya kubadilisha mwili wake uwe kama ulivyokuwa sasa haijakuwa hatua rahisi .

Aliwashauri wanadada ambao wangetaka kufanyiwa upasuaji wa kimwili kuukubali mwili wao na kubaki walivyo kwani itawaletea shida huko mbeleni.

"Wanadada tafadhalini, mjue kujipenda mlivyo na msikubali shinikizo la rika liwafanye mkimbilie kufanya mambo ambayo yatawaharibia maisha yenu huko mbeleni," alisema.

Sidika alisema kuwa yalikuwa maajabu na kuwa alikuwa na bahati kuwa hai baada ya mwili huo wake wa zamani kumleta shida ya kiafya.

Alisema kuwa mambo hayakuwa rahisi kabla aende kwenye upasuaji wake na hata alipoenda alimshukuru Mungu kwa kumpa zawadi ya uhai na afya njema.

Mjasiri mali huyo aliongeza kuwa amejikubali alivyo na amejifunza kuizoea hali hiyo ya mwili wake mpya na hata nini itendeke ataendelea kujipenda alivyo sasa.

Hii imetendeka baada ya siku yake ya kuzaliwa kupita hivi majuzi na mwanasosholaiti huyo kusherehekea kuwa kuzaliwa upya.

"Nina bahati kuwa hai. Sikusherehekea siku yangu ya kuzaliwa mwaka huu, lakini tuko hapa sasa. Heri ya kuzaliwa kwangu. Nimekuja kushukuru kuwa na uhai na kutoyachukulia mambo yoyote hivihivi," alisema mama huyo.

Aliwaambia mashabiki wake kuwa bado yeye wa sasa hivi ni yule yule Sidika aliye mzuri na hajabadilika kivyovyote vile.

Sidika aliwashukuru mashabiki wake kwa kumuunga mkono na kumwonyesha upendo na aliwahimiza wamsaidie kwa safari hii yake mpya.

"Naishukuru familia yangu haswa mume wangu kwa kuwa na mimi kwa wakati huu mgumu, na hata nyinyi mashabiki wangu," alisema.

Alisema ataanika mtandaoni video za upasuaji wake ili kuweza kuwashinikiza wale ambao wangetaka kufanyiwa upasuaji wa kubadilisha mwili wao wasijaribu kufanya hilo.