West Pokot: Polisi wapigwa mawe baada ya kuvamia banda la mchezo wa Pooltable

Polisi wawili walijeruhiwa vichwani kwa mawe huku mwingine akiumizwa mdomo na kung'oka meno

Muhtasari

• Maafisa hao walivamia chumba kimoja katika mji wa Makutano ambapo takriban watu 20 walikuwa wakicheza mchezo wa pooltable

Kituo cha polisi cha Kapenguria
Kituo cha polisi cha Kapenguria
Image: Maktaba

Katika kaunti ya West Pokot, polisi walioneshwa kilichomnyoa kanga manyoya baada ya kutaka kuwatia mbaroni vijana ambao waliwageukia na kukabiliana nao katika vita kali.

Kulingana na jarida la Nation, maafisa hao walikuwa wameenda kuwakamata washukiwa wanaodaiwa kuwatisha watu katika mji wa Kapenguria na viunga vyake.

“Maafisa hao walivamia chumba kimoja katika mji wa Makutano ambapo takriban watu 20 walikuwa wakicheza mchezo wa pooltable. Vijana hao walichukua tahadhari na kuanza kuwarushia mawe maafisa hao,” Nation waliripoti.

Maafisa hao walipata majeraha na kupelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Kapenguria ambapo wawili kati yao walijeruhiwa baada ya kupigwa kwa mawe vichwani. Afisa wa tatu alipigwa mdomoni na kuvunjika meno tatu.

Kamanda wa polisi katika kaunti hiyo ya West Pokot Peter Kattam aliiambia Nation kuwa maafisa wake walifanikiwa kuwakamata vijana kadhaa na bado msako ungali unaendelea kuwatafuta wahusika zaidi ambao waliwavamia polisi.

Bw Kattam aliwataka wenyeji kushirikiana na maafisa wa polisi kuwakamata wahalifu zaidi walioko mbioni na kudumisha sheria na utulivu.

"Inasikitisha wenyeji waliamua kupambana na polisi, jambo ambalo liliwapa wahalifu fursa ya kutoroka" alinukuliwa.

Aliongeza kuwa wahalifu sita walikuwa kwenye rada ya polisi na walikuwa wakifuatiliwa.