Miguna ataka kumng'atua Odinga kama msemaji wa Nyanza, je atawezana?

Katika msururu wa tweets zake, Miguna amekuwa akidokeza kwamba sasa yeye ndiye wa kutoa muongozo kwa watu wa Nyanza kisiasa.

Muhtasari

• Baada ya kurejea kutoka uhamishoni, Miguna alisema kwamba hivi karibuni atatoa muongozo wa kisiasa kwa watu wa Nyanza.

Miguna apanga njama ya kumng'atua odinga kama msemaji wa Nyanza
Miguna apanga njama ya kumng'atua odinga kama msemaji wa Nyanza
Image: Maktaba

Wakili mwenye tantarira nyingi, Miguna Miguna anaonekana kujiweka katika nafasi ya kuanzisha njama ya kuchukua ubabe katika eneo la Nyanza kama mrithi wa Raila Odinga.

Katika msururu wa tweets zake, Miguna tangu kutua nchini Oktoba 20 amekuwa akidokeza njama ya kutaka kumng’oa Odinga kama mbabe wa kisiasa wa Nyanza na nafasi hiyo kuikaba yeye.

 Kwa mara kadhaa amekuwa akidokeza kuwa msukumo huo hautokani na yeye binafsi bali ni wananchi na haswa wenyewe kutoka mkoa huo ambao wanamsukuma kuwa msemaji wao wa kisiasa.

“Kila mahali ninapoenda, Wakenya kutoka tabaka mbalimbali huniambia: ‘Asante kwa kutokuwa na woga na uthabiti na kwa kupigana vikali dhidi ya wadhalimu wasio na haki. Ndugu wadhalimu wameipora nchi hadi kufa. Tunatumai utaendelea kupigania waporaji waadhibiwe!” Miguna alisema katika moja ya tweet yake.

Katika muendelezo huo, wakili huyo mwenye utata pia alizidi kusema kuwa wikendi iliyopita alikutana na baadhi ya vijana kutoka jamii ya Luo viungani mwa jiji la Nairobi waliomshangilia na kumpa himizo kuwa yeye ndiye wanategemea uwanyooshea mambo.

“Mapema leo, nilipokuwa nikitembea-tembea kuzunguka Hurlingham, Nairobi, kikundi cha Wajaluo walinivamia wakisema: “Jatelo! Wewe ndiye sasa tunaweka matumaini yetu kwako. Safari ya Jakom imefikia mwisho!” Uungwaji mkono na mshikamano kutoka kwa Wakenya wote umekuwa wa unyenyekevu na mwingi sana!” aliandika.

Miguna hivi majuzi alirejea Kenya baada ya miaka minne uhamishoni kutokana na kuzozana na utawala wa rais wa zamani Uhuru Kenyatta. Katika siku za hivi karibuni alisema atatoa 'maelekezo' kwa jamii yake ya Waluo.

Je, ataweza kumng’oa Odinga kama msemaji wa wajaluo kisiasa?