'Nilimshinda Museveni katika uchaguzi wa Urais wa Uganda,'Bobi Wine adai

“Nilimshinda Jenerali Museveni, kila mahali nchini. Sahau hiyo tume ya uchaguzi ya udanganyifu.

Muhtasari
  • Aliorodhesha zaidi kukatika kwa mtandao pamoja na madai ya kutoonyeshwa waangalizi wa uchaguzi kutoka mataifa na mashirika ya kigeni

Kiongozi wa chama cha upinzani nchini Uganda cha National Unity Platform (NUP) Robert Kyagulanyi, almaarufu Bobi Wine, amedai kuwa alimshinda kiongozi wa muda mrefu wa nchi hiyo Yoweri Museveni kura katika uchaguzi wa urais nchini humo mwezi Januari mwaka jana.

Akiwa kwenye mahojiano na runinga ya Citizen Wine aliendelea kudai kuwa hata hivyo hakutangazwa kuwa rais wa nchi na tume yao ya uchaguzi kutokana na dosari katika mchakato mzima wa upigaji kura unaodhaniwa uliandaliwa na ‘mzee mwenye kofia,’ kama Museveni anavyojitaja mara kwa mara.

Aliorodhesha zaidi kukatika kwa mtandao pamoja na madai ya kutoonyeshwa waangalizi wa uchaguzi kutoka mataifa na mashirika ya kigeni kama vile Marekani na Umoja wa Mataifa, kama sababu zaidi kwanini uchaguzi ulivurugwa.

“Nilimshinda Jenerali Museveni, kila mahali nchini. Sahau hiyo tume ya uchaguzi ya udanganyifu. Hakukuwa na uhalali wowote; kila chombo cha sheria na sheria ilipuuzwa. Hii ni kampeni ya urais ambapo nilitekwa nyara siku ya kuteuliwa kwangu, Desemba 2020, na timu yangu yote ilikamatwa,” alisema.

"Tulienda kwenye uchaguzi huo mtandao ukiwa umezimwa kabisa, wanajeshi kila mahali, waangalizi wetu wote wa uchaguzi walikusanywa, waangalizi wa uchaguzi wa Marekani na Umoja wa Mataifa hawakujitokeza, huwezi kuitisha uchaguzi huo. Lakini pamoja na hayo, tulifanikiwa kumpiga Jenerali Museveni.”

Kulingana na Wine, lengo lake kuu ni kuwakomboa tu raia wa Uganda, haswa vijana, ili waweze kuamsha uwezo wao na kuhakikisha kuwa kura zao zinahesabiwa.