Ruto azungumzia picha ya kukutana na Uhuru Kenyatta, "Nilimsalimia, nikamtazama machoni"

Rais Ruto pia alimpongeza mtangulizi wake kwa kuongoza mazungumzo ya amani nchini DRC.

Muhtasari

• Katika hotuba yake, Ruto alimmiminia Uhuru sifa nyingi, akisema rais huyo wa zamani, amefanya kazi kutnu kuongoza mazungumzo ya amani DRC.

Viongozi wa ukanda wa EAC wakiongozwa na rais William Ruto
Viongozi wa ukanda wa EAC wakiongozwa na rais William Ruto
Image: Facebook

Kwa mara ya kwanza rais William Ruto amezungumzia jinsi walivyokutana na mtangulizi wake rais mstaafu Uhuru Kenyatta Jumatatu katika Hoteli ya Safari Park jijini Nairobi.

Wawili hao walikutana hadharani kwa mara ya kwanza tangu Kenyatta alipomkabidhi Ruto vyombo vya madaraka ugani Kasarani mnamo Septemba 13 wakati wa kuapishwa kwake.

Mkutano wao ulikuwa unazungumzia hatua ambazo zimepigwa katika kudumisha Amani kwenye ukanda wa Afrika Mashariki na haswa taifa la DRC ambalo ni mwanachama mpya wa muungano wa EAC.

Mkutano huo ulikuwa wa tatu katika kutolea tathmini ya hatua ambazo mataifa ya eneo hili yamepiga katika kuhakikisha Amani inarejeshwa katika upande wa mashariki mwa Kongo, eneo linalokumbwa na mizozo ya vita baina ya vikosi vitiifu vya serikali na vikosi vya waasi wa M23 kwa muda mrefu sasa.

Ruto alimpongeza mtangulizi wake kwa kukubali kuchukua jukumu la kuongoza mazungumzo ya Amani baina ya pande husika katika taifa hilo, na alisema mara ya kwanza alikutana na Kenyatta alimsalimia, akamtazama usoni na kumtamkia pongezi hizo.

“Nilikutana na mheshimiwa rais, nikamtazama machoni na kumwambia, 'Mheshimiwa Rais, umeanza mchakato muhimu sana katika EAC, ningependa uendelee na mchakato huo', akaniambia yuko tayari kuufanya,” rais Ruto alisema.

Katika hotuba yake, Ruto alimmiminia Uhuru sifa nyingi, akisema rais huyo wa zamani, mwezeshaji wa mchakato wa amani wa EAC, amefanya kazi nzuri katika kutafuta amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

“Licha ya yote yaliyoendelea, kwa sababu ya maslahi ya taifa letu, kanda na bara letu, na kwa sababu amani ni muhimu kwa Kenya, DRC na kwa eneo letu, Rais Kenyatta amefanya kazi nzuri anapowezesha mchakato huu. Kwa sababu kwa pamoja kama nchi tunathamini amani,” alisema.