Mbunge Elachi amhurumia gavana Mwangaza hoja ya kubanduliwa ikipitishwa

Jumatano MCAs 67 kati ya 69 walipitisha hoja ya kumbandua Mwangaza kama gavana.

Muhtasari

• Hoja hiyo tayari imewasilishwa kwa spika wa bunge la seneti na Mwangaza atalazimika kujitetea mbele ya maseneta ili kuweka hai matumaini yake kuendelea kuwa gavana.

GAVANA WA MERU KAWIRA MWANGAZA
Image: KAWIRA MWANGAZA/FACEBOOK

Mbunge wa Dagoretti ya Kaskazini Beatrice Elachi amemhurumia gavana wa Meru Kawira Mwangaza baada ya MCAs wa bunge la kaunti hito kupitisha hoja ya kumbandua mamlakani.

Jumatano joni, MCAs 67 kati ya 69 wa kaunti hiyo walipiga kura ya ndio kutaka Mwangaza kung’atuliwa kama gavana kwa kile walikitaja kuwa ni matumizi mabaya ya ofisi na pia kumpa mumewe, Baichu kazi katika ofisi ya kaunti.

Matumaini ya Mwangaza kuendelea kuwa gavana wa kaunti hiyo sasa yamening’inia katika bunge la seneti ambalo linatarajiwa kupitisha aqu kuangusha hoja hiyo.

Elachi akizungumza katika mahojiano ya kituo cha runinga NTV asubuhi ya Alhamisi, alisema kuwa anamhurumia Mwangaza na anahisi kwamba hangepitia mchakato huo wa kubanduliwa.

Kulingana na Elachi, Kawira atazuiwa kupata pesa za kaunti na hivyo kufanya iwe vigumu kwake kutekeleza ahadi zake za kampeni za uchaguzi.

“Laiti angeepuka kufunguliwa mashtaka, Mwangaza alikuwa na njia mbili za kukwepa. Alipaswa kukaa tu na MCAs na kusikiliza. Wakati mwingine tunashuka na kusikiliza. Natamani angetumia maarifa yake ya mimbari, kuwashirikisha MCAs katika uongofu ili kukubaliana nao,” alisema.

Gavana huyo wa Meru ndiye Gavana wa kwanza kuondolewa madarakani tangu Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9.

"Waheshimiwa wanachama, ningependa kutangaza kwamba Gavana wa Meru Mhe. Askofu Kawira Mwangaza ameng’atuliwa na Bunge la Kaunti ya Meru," Spika wa Kaunti ya Meru Ayub Bundi Solomon alisema.

Taarifa za hivi punde ni kwamba hoja hiyo ya kumbandua iliyopitishwa na MCAs tayari imewasilishwa kwa spika wa bunge la seneti.