Kwa mara ya kwanza Wajackoyah aonekana bila kitambaa maarufu cha kichwani

Alisema kitambaa hicho alimpa kama zawadi kijana mmoja aliyechora picha yake.

Muhtasari

• Wajackoyah ni miongoni mwa watu ambao wamezoeleka pakubwa kwa kuvalia kitambaa hicho kama nembo ya utambulisho wao.

• Wengine ni wasanii Redsan na Nameless amabo pia hawajawahi onekana bila durag hiyo ya kichwani.

Wajackoyah na familia yake
Wajackoyah na familia yake
Image: Facebook

Hivi umewahi jiuliza itakuwaje siku moja mkikutana na msanii Nameless bila kitambaa chake cha kichwani ambacho ni kama nembo ya utambulisho wake?

Na vipi kuhusu watu wengine kama aliyekuwa mgombea urais wakili msomi George Wajackoyah kumkuta bila kile kitambaa cha kichwani mwake?

Ukweli ni kwamba ni jambo la bashasha na kushangaza kuwaona watu uliokuwa unawazoea wakiwa na baadhi ya nembo za mionekano yao wakiwa wamebadili kwa namna moja au nyingine.

Wajackoyah amekuwa gumzo la mitandaoni baada ya kuonekana kwa mara ya kwanza tangu ajulikane mitandaoni kutokana na azma yake ya kuwania urais. Wakili huyo alionekana pasi na kitambaa cha kichwani mwake na wafuasi wake hawakukimya kuzungumzia muonekano wako wa kitofauti kabisa.

Mnamo Desemba 25, 2022, Wajackoyah, aliingia kwenye mitandao ya kijamii na kuweka picha zake akiwa hana durag, akifichua kuwa alimzawadia msanii mchanga ambaye alikuwa amechora picha yake ya kichwa.

“Kijana huyu alistahili heshima yangu. Alikaribishwa katika udugu baada ya kuchora picha yangu. Alipoulizwa anataka nini, alisema simu na matakwa yake yamekubaliwa,” Wajackoyah alisema.

Wajackoyah aliendelea kutumia siku ya Krismasi bila durag huku akipiga picha na familia na marafiki kadhaa.

Wafuasi wake walishangazwa na muonekano huo wengine wakifunguka kuwa muda wote wamekuwa wakidhani ni mtu mwenye kulea nywele ndefu aina ya rasta lakini wakashangaa kuona ni mtu mwenye nywele fupi tu kawaida.

Wajackoyah alijizolea umaarufu alipozindua manifesto yake ya kuwania urais akipigia upato uhalalishwaji wa bangi pamoja na kuuza nyama ya mbwa na fisi kwa taifa la Uchina.