Alai aitisha uchunguzi dhidi ya mauaji ya mwana-LGBTQ, "Alikuwa anaishi maisha yake!"

"Alikuwa akiishi maisha yake tu. Kwa nini kumuua?” Alai aliuliza.

Muhtasari

• Alai pia alitaka rais Ruto na DCI kutoa tamko lao kuhusu mauaji hayo.

• Mwili wa Chiloba ulipatikana siku chache nyuma ukiwa umewekwa ndani ya sanduku la chuma na kutupwa barabarani.

Mwanaharakati wa LGBTQ, Edwin Chiloba
Mwanaharakati wa LGBTQ, Edwin Chiloba
Image: Instagram

Diwani wa Kileleshwa jijini Nairobi Robert Alai amekuwa mtu wa hivi karibuni kushtum kisa cha mauaji ya mwanachama wa jamii ya mashoga na wasagaji, LGBTQ, mwanafasheni Edwin Chiloba.

Chilomba alitambuliwa Alhamisi usiku, siku kadhaa baada ya mwili wake kupatikana umetupwa barabarani katika kaunti ya Uasin Gishu ukiwa umewekwa ndani ya sanduku la mabati, na tayari ulikuwa umeanza kuoza.

Baada ya kugundulika kuwa mwili huo ulikuwa wa mwanaharakati huyo wa LGBTQ ambaye pia alikuwa anajiongeza kama mwanamitindo wa fasheni, watu mbalimbali wameshtumu mauaji hayo ambayo yamehusishwa na misimamo yake mikali dhidi ya wale waliokuwa wanakashfu jamii ya watu wa mapenzi ya jinsia moja.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, mwakilishi wadi Alai alikashfu kitendo cha mauaji hayo na kutaka uongozi na idara ya upelelezi wa jinai kufanay uchunguzi wa kina ili kubaini waliotenda unyama huo.

Alai alisema kuwa vitendo vya kuua mtu kutokana na misimamo yake kijinsia au kimapenzi vimepitwa na wakati kwani katika dunia ya sasa, kila mtu anafaa kupewa uhuru wa kuchagua maisha yake pasi na kutishiwa kwa njia yoyote.

“Mauaji ya mwanaharakati wa LGBTQ Edwin Chiloba LAZIMA yachunguzwe na wahusika kushtakiwa mahakamani. Hili LAZIMA lisitokee tena. Alikuwa akiishi maisha yake tu. Kwa nini kumuua?” Alai alisema.

Pia mwanasiasa huyo ambaye pia ni mwanablogu aliwataka rais William Ruto na idara ya upelelezi wa jinai DCI kutoa tamko rasmi kuhusu mauaji hayo.

Chiloba alipatikana ameuawa na mwili wake kuhifadhiwa kwenye sanduku la chuma kando ya barabara ya Kipenyo-Kaptinga, huko Kapsaret, Uasin Gishu.

Polisi walisema taarifa za awali zinaonyesha gari lisilo na idadi lilionekana likidondosha boksi la chuma eneo hilo na mwendesha Bodaboda aliyetokea eneo hilo wakati likitokea.