Marekani yataka kujumuishwa katika uchunguzi wa mauaji ya Edwin Chiloba wa LGBTQ

"Ikiwa kuna chochote tunaweza kufanya kusaidia, tuko tayari kufanya hivyo" - Msemaji wa mambo ya nje wa USA.

Muhtasari

• Msemaji wa mambo ya nje wa Marekani Ned Price ni miongoni mwa watu ambao wameweka wazi kwa muda mrefu kuwa ni wanachama wa LGBTQ.

Mwanaharakati wa LGBTQ, Chiloba
Mwanaharakati wa LGBTQ, Chiloba
Image: Instagram

Jarida moja la Marekani linalosukuma mbele ajenda za wapenzi wa jinsia moja na jamii nzima ya LGBTQ, kwa jina Washington Blade limesema kuwa Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani Ned Price ametoa wito kwa Kenya kuihusisha Marekani katika uchunguzi wa mauaji ya Edwin Kiprotich Kiprop almaarufu Chiloba ambaye alikuwa mwanaharakati wa LGBTQ nchini.

Kulingana na jarida hilo, Price alitoa wito kwa idara za uchunguzi nchini kufanya mchakato wa kubaini kiini cha mauaji ya mwanaharakati huyo kwa njia ya umakini mkubwa ili kuhakikisha kuwa wahusika wote wanachukuliwa hatua madhubuti.

“Tunawaomba na kutarajia Wakenya kufanya uchunguzi wa kina na wa uwazi kuhusu kifo chake," Price, ambaye ni shoga waziwazi, aliambia Washington Blade wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari kila siku. "Na kwa kweli ikiwa kuna chochote tunaweza kufanya kusaidia, tuko tayari kufanya hivyo."

Msemaji huyo alitoa rambirambi zake kwa familia ya Chiloba pamoja na jamii nzima ya LGBTQ huku akisisitiza kuwa wataendelea kufuatilia uchunguzi huo kwa ukaribu mno. Pia alikemea visa vya unyanyasaji dhidi ya wanajamii wa LGBTQ licha ya madai kuibuka upya kuwa Chiloba hakuuawa kutokana na misimamo yake ya kutetea mapenzi ya jinsia moja bali ni kutokana na mzozo wa kimapenzi.

“Tunatuma risala zake za rambirambi kwa familia yake, kwa wapendwa wake lakini pia kwa jamii ya LGBTQI+ nchini Kenya wakati wa maombolezo yao. Kuna watu wengi sana katika jamii hiyo nchini Kenya ambao walinufaika na uongozi wake, kutokana na kuonekana kwake, kutokana na usaidizi wake."

"Unyanyasaji dhidi ya watu wa LGBTQI+ - au mtu yeyote, bila shaka - haukubaliki, lakini vurugu inapotokana na uwezekano wa upendeleo au unyanyapaa, inadhuru kwa njia isiyo ya moja kwa moja wanachama wote wa jamii inayolengwa," alinukuliwa na jarida la Washington Blade.

Chiloba alipatikana ameuawa na mwili wake kusondekwa ndani ya sanduku la chuma wiki moja iliyopita, jambo ambalo limegonga vichwa vya habari kote duniani.