Kisa cha mvulana wa chuo kikuu aliyefariki baada ya kuomba Ksh 150 kununua maandazi

Mpenzi wake alisema marehemu alimpigia simu kumuomba shilingi 150, alipomwambia hana, alikata simu.

Muhtasari

• Mpenzi wake alieleza kuwa baada ya kumwambia hakuwa na shilingi 150 alizomuomba, Gregory alikata simu na siku moja baadae mwili wake ukapatikana ndani ya nyumba.

• Wawili hao walikuwa na mtoto mmoja lakini hawakuwa wanaishi pamoja.

Mwili wa marehemu
Mwili wa marehemu
Image: Instagram//Azam

Mwanafunzi wa chuo kikuu cha TUM jijini Mombasa alipatikana amefariki katika hali ya kutatanishi saa chache tu baada ya kumpigia mpenzi wake simu akimuomba pesa za kununua vitumbua.

Inaarifiwa kuwa mwanafunzi huyo Gregory Mutinda mwenye umri wa miaka 24 alipatikana amefariki ndani ya nyumba yake na mpenzi wake alieleza vyanzo vya habari kwamba alikuwa amempigia simu kumuomba shilingi 150 za kununua maandazi.

Baada ya mpenzi huyo kumweleza kwamba hakuwa na pesa hizo, Gregory alikata simu na saa chache baadae Mercy ambaye ni mpenzi wake alipomtembelea alimpata sakafuni akiwa maiti.

Mutinda na mpenzi wake Mercy walikuwa na mtoto mmoja wa kiume na inaarifiwa siku moja kabla ya tukio hilo, alikuwa nyumbani kwa mpenzi wake.

“Sikuwepo siku hiyo. Lakini pamoja na rafiki yake walitembelea mahali pangu na kukaa siku nzima na mtoto wetu. Akilini nilijua kila kitu kiko sawa. Siku iliyofuata tulizungumza asubuhi na mapema mwendo wa saa tatu asubuhi na kumuuliza ikiwa anaenda mahali pa kazi ambapo alikuwa akifanya kazi. Alijibu kwa kishindo na tukaagana,” akasema Bi Mercy.

Alisema kuwa baada ya Mutinda kukata simu, dakika chache baadae alimpigia tena safari hii akiwa na ombi la ajabu la kuomba angalau shilingi 150 kwa ajili ya vitumbua.

“Sikuwa na pesa kwenye Mpesa yangu hivyo nikamwambia sina pesa, akanyamaza na kukata simu. Mnamo saa tano asubuhi nilimtumia Gregory ujumbe lakini haukuwasilishwa. Saa tisa nikampigia bado hakuchukuwa na hajawahi kosa kupokea simu yangu, nikaingiwa na wasiwasi na kumpigia rafiki yake ambaye aliniambia hajakutana naye,” akaeleza Bi Munyao.

Mwanadada huyo aliamua kunyata mwenyewe hadi kwa nyumba alimokuwa akiishi mpenzi wake na kuchungulia kutoka dirishani alimuona amelala sakafuni akiwa hana uhai.

Polisi sasa wanachunguza kisa hicho ili kubaini kama kuna uwezekano wa kuuawa au kujitoa uhai.