Spika Kingi amfukuza seneta wa Kitui Enock Wambua bungeni kwa 'mavazi yasiyofaa'

Seneta Wambua alikuwa anawasilisha hoja kwa njia ya mtandaoni akiwa amevalia jezi ya Kenya.

Muhtasari

• Spika alimwambia Wambua kuvalia vizuri lakini akasema kuwa pahali alipokuwa mtandao haungemruhusu kufanya hivo.

• Kutokana na hilo, spika Kingi alimsikitikia na kumwambia kuwa hangeweza tena kuendelea kuwasilisha hoja yake.

Spika Kingi amfurusha seneta Wambua bungeni kwa kuvaa visivyo
Spika Kingi amfurusha seneta Wambua bungeni kwa kuvaa visivyo
Image: Twitter

Seneta wa Kitui Enock Wambua alilazimika kufungiwa kutoka kuwasilisha hoja yake katika bunge la seneti baada ya spika Amason Kingi kugundua kuwa alikuwa amevalia kwa njia ambayo aliitaja kuwa isiyofaa.

Awali, Spika Amason Kingi alikuwa amemruhusu Seneta huyo kuendelea lakini akamkatisha kwa vile kamera yake ilikuwa imezimwa. Alipowasha kamera, Karani alimwendea Spika na alionekana akimnong'oneza kabla ya Spika kumfukuza Seneta Wambua.

Seneta Wambua hakuwa bungeni wakati wa kikao hicho Alhamisi asubuhi na alikuwa anawasilisha hoja yake kupitia njia ya mtandao.

Baada ya karani kumnong’onezea spika, ghafla alimtaka Wambua kuwasha kamera na seneta huyo alionekana akiwa amevalia jezi yenye bendera ya Kenya.

“Washa kamera yako. Tunahitaji kuona ulipo, na unajua unahitaji kuvalia ipasavyo,” Seneta alisema.

"Bw Spika nataka kufanya hivyo lakini mtandao hautaendeleza hilo," Seneta Wambua alijibu.

Kamera ilipowashwa, Seneta huyo alionekana akiwa amevalia jezi yenye bendera ya Kenya jambo lilizozua minong’ono kutoka kwa baadhi ya maseneta ambao walitaka alifungiwe kuendelea.

“Bwana Spika hili ni vazi la Kenya. Hii ni bendera ya Jamhuri ya Kenya, Mheshimiwa Spika,” Wambua alijariu kujitetea lakini machozi yake yalienda na maji.

Spika Kingi alimkatalia kabisa na kumfurusha.

“Seneta Wambua, ukweli tu kwamba kuwa na bendera hakufanyi ufikie kanuni za mavazi inavyotakiwa na kiwango cha Seneti. Labda unaweza kuendelea na uwanja wa Soka. Kwa hivyo ninahofia Seneta Wambua huenda usiendelee kutoa mchango wako kwa sababu hujavalia ipasavyo.”