Raila na Orengo waliokoa maisha yangu-Wajackoyah afichua

Alisema ni wakati huo ambapo Robert Ouko aliuawa.

Muhtasari
  • Akizungumza katika eneo la Kamukunji siku ya Jumatatu, Wajackoyah alisema kuwa Raila na mshirika wake wa muda mrefu James Orengo waliokoa maisha yake
Wajackoyah amtaka Raila kustaafu
Wajackoyah amtaka Raila kustaafu
Image: Maktaba

Kiongozi wa chama cha Roots na wakili George Wajackoyah sasa anasema yu hai leo, kwa sababu ya juhudi za kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Akizungumza katika eneo la Kamukunji siku ya Jumatatu, Wajackoyah alisema kuwa Raila na mshirika wake wa muda mrefu James Orengo waliokoa maisha yake wakati utawala wa Kanu ulipomfuata.

Orengo ndiye Gavana wa sasa wa Siaya.

"Niko hapa kwa sababu ya Raila. Ninaishi leo kwa sababu ya Raila. Ikiwa Raila hangekuwapo, nisingepata fursa ya kuwa hai leo. Raila na James Orengo waliokoa maisha yangu. Baba aliniokoa wakati nilikuwa nauawa na ile serikali ya wakatili," alisema.

Wajackoyah aliongeza kuwa ni Raila na kisha Balozi wa Marekani nchini Kenya, Smith Hempstone waliofanya kazi ili asafirishwe nje ya nchi.

Alisema ni wakati huo ambapo Robert Ouko aliuawa.

Wajackoyah alizungumza hayo wakati wa mkutano wa Kamukunji ambapo viongozi wa Azimio walidai kwamba Raila alishinda katika uchaguzi wa Urais wa mwaka jana.