Hakuna aliyepanga njama ya kumuua Chebukati-Raila ajibu madai ya Rais Ruto

"Hakuna aliyepanga njama ya kumuua Chebukati, ikiwa Ruto ana ushahidi anapaswa kuupeleka kwa polisi

Muhtasari
  • Akiongea Jumatatu wakati wa mkutano wa Azimio huko Kamukunji, Raila alisema kuwa Ruto kama Rais hana uwezo wa kutoa matamshi kama hayo
RAILA ODINGA
Image: ANDREW KASUKU

Kiongozi wa Azimio Raila Odinga amemkashifu Rais William Ruto kuhusu madai ya njama ya kumuua Chebukati.

Akiongea Jumatatu wakati wa mkutano wa Azimio huko Kamukunji, Raila alisema kuwa Ruto kama Rais hana uwezo wa kutoa matamshi kama hayo.

"Hakuna aliyepanga njama ya kumuua Chebukati, ikiwa Ruto ana ushahidi anapaswa kuupeleka kwa polisi kwa uchunguzi ili waliohusika wakamatwe. Ilikuwa ya kisiasa," akasema.

Raila alisema kuwa madai hayo ya Ruto yalichochewa kisiasa.

Hii ni baada ya Ruto kudai kuwa kulikuwa na njama ya kumteka nyara, kumtesa na kumuua Chebukati katika Bomas of Kenya.

Inadaiwa kuwa njama ya mauaji ya Chebukati ilifichuliwa na Ruto mwanzoni mwa wiki wakati wa mkutano na chifu anayeondoka wa IEBC na makamishna wengine katika Ikulu ya Nairobi.

Njama hiyo, alisema, ilibuniwa na muungano wa kisiasa ambao ulikuwa ukisimamia urithi wa urais kama hatua ya mwisho ya kulazimisha mgombea wao anayependelea dhidi ya Wakenya.