Mwili wa mwanamke wa ujauzito wa miezi 4 wapatikana uchi, umedungwa visu mgongoni

Alinyongwa na kuvunjwa mikono, kabla ya kutupwa uchi, sehemu zake za siri zikifunikwa na jani la mgomba.

Muhtasari

• Katika nyumba ya mshukiwa, kulikuwa na matone ya damu na alama za kukokota zikiashiria aliuawa hapo kabla ya kuutupa mwili wake nje.

Mwanamke mjamzito apatikana amedungwa visu mgongoni
Mwanamke mjamzito apatikana amedungwa visu mgongoni
Image: Maktaba//The Star

Wakazi wa kijiji cha Mwanzai Kaloleni kaunti ya Kilifi walipigwa na butwaa baada ya kuupata mwili wa mwanamke mmoja mjamzito akiwa uchi wa hayawani.

Kulingana na taarifa, wakazi waliokuwa wamehudhuria mazishi walipewa tangazo kuwa kuna mwili umepatikana ndani ya shamba la migomba ukiwa uchi na usaidizi ulihitajika ili kuutambua.

Nation walisema mwili huo ulitambuliwa kama wa mwanamke mmoja kwa jina Risper Chizi, mwanamke wa miaka 26 ambaye alikuwa tayari na ujauzito wa miezi 4 na alikuwa amefumwa visu kadhaa mgongoni.

Polisi walisema kuwa mumewe mwenye miaka 22 ndiye mtuhumiwa nambari moja kwani alitoweka na hajapata kuonekana tangu tukio hilo la Jumamosi wiki iliyopita.

“Uchunguzi wa awali unaonyesha muuaji au wauaji wake walimnyonga na pia kumvunja mikono. Zaidi ya hayo, alikuwa na michubuko kwenye magoti na sehemu za siri zilizofunikwa na jani la mgomba,” Jarida la Nation liliripoti.

Mkuu wa polisi katika Kaunti Ndogo ya Kaloleni Alexander Makau alithibitisha kisa hicho na kusema kuwa mume ndiye mshukiwa mkuu. Bw Makau alisema mume huyo alitoroka baada ya mauaji hayo.

Familia ya kina Chizi ilidhibitisha kuwa wanandoa hao walikuwa na ugomvi wa mara kwa mara na huenda mumewe alimuuwa baada ya kuzozana kama ilivyokuwa kawaida yao.

Katika nyumba ya mshukiwa, kulikuwa na matone ya damu na alama za kukokota, zikiashiria kuwa mwanamke huyo huenda aliuawa ndani ya nyumba hiyo na kutupwa mahali pengine.

Uchunguzi wa maiti kubaini chanzo cha kifo hicho utafanywa Jumatatu katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Kilifi.