Mlevi ashambuliwa hadi kufa kwa kujichanganya na kuingia nyumba ya jirani kimakosa

Mwanamume huyo mlevi alijichanganya na kuingia nyumba ya jirani yake mwanamke aliyepiga kelele kuita watu.

Muhtasari

• Baada ya mwanamke huyo kupiga mayowe, majirani waliitikia kwa haraka na kufika ambapo walimpa mlevi kipigo.

• Polisi walifika eneo la tukio na kumchukua hospitali alipofariki kutokana na majeraha.

Polisi katika eneo la Dagoretti jijini Nairobi wanachunguza kisa ambapo mwanamume mmoja mlevi alishambuliwa hadi kufa baada ya kujichanganya na kuingia nyumba ambayo haikuwa yake kimakosa.

Zogo lilizuka baada ya mwanamke mwenye nyumba hiyo kuanza kupiga kelele akiita watu kuwa mwanamume huyo mlevi alikuwa analeta usumbufu nyumbani mwake, katika kile kilichoonekana kama kudhania alikuwa nyumbani mwake.

"Ugomvi ulitokea ambapo mwanamke aliyekuwa na hofu aliamsha majirani zake na wakajibu kwa kumshambulia jamaa huyo," ripoti hiyo ilisoma kwa sehemu kulingana na jarida moja la humu nchini.

Aliokolewa na kupelekwa katika Hospitali ya Eagles, ambapo alifariki dunia baadae kutokana na majeraha mabaya aliyoyapata kutokana na kipigo cha halaiki.

Tukio hilo linaendelea kuchunguzwa na maafisa wa upelelezi ambao sasa wanamhusisha mpaka mwanamke mwenye nyumba hiyo pamoja na majirani wa kwanza walioitikia kamza, huku mwili mwa mwanamume huyo ukipelekwa katika makafani.

Haya yanajiri siku moja tu baada ya Miili ya mama na mwanawe kupatikana katika nyumba yao eneo la Kabete, kaunti ya Kiambu baada ya kudaiwa kujitoa uhai.

Polisi walisema Ruth Nyambura Karuga, 32, alikuwa ametoweka katika eneo lake la kazi kabla ya kugunduliwa akiwa amekufa nyumbani kwake katika mtaa wa Nyathuna siku ya Alhamisi, Januari 26.

Kando na mwili wake uliokuwa juu ya kitanda, ulilala mwili wa mtoto wake Francis Kinyanjui, 11.