Machifu 10 watuhumiwa kushirikiana kuzamisha vijana 2 mtoni hadi kufa, familia zalilia haki

Inadaiwa machifu 2 na manaibu chifu 8 waliwatumbukiza vijana hao kwenye mto wa Chania wakiwa na pingu mikononi.

Muhtasari

• Machifu walisema vijana hao walikuwa wagemaji wa Chang'aa ambao walijitupa mtoni baada ya kuona wanaiwa mbaroni.

• Wanakijiji walioshuhudia walisema vijana hao walikuwa wavuvi ambao walisukumwa mtoni wakiwa wamefungwa pingu.

Crime Scene
Image: HISANI

Taarifa zinadai kwamba machifu 2 na machifu wasaidizi 8 walidaiwa kuungana na kutupa vijana wawili mtoni wakiwa wamefungwa pingu wangali bado hawajafunguliwa mashtaka.

Kisa hicho ambacho kiligonga vichwa vya habari mwaka 2019 katika kaunti ya Murang’a kingali bado kinafuatiliwa na familia za vijana hao ambao walikufa maji mpaka sasa huku wakililia haki kwa wanao.

Inadaiwa kwamba vijana hao wawili marehemu Nicholas Maithya mwenye umri wa miaka 20 na mwenzake Asman Kamau wa miaka 18 walifungwa pingu na machifu hapo kabla ya kutupwa kwenye mto Chania, katika kijiji cha Rubiro kaunti ya Murang’a.

Miili yao ilipatikana siku nane baadae ambapo taarifa zilizowasilishwa kwa vyombo vya sheria zikikinzana vikali kutoka kwa machifu hao na wanakijiji walioshuhudia.

Kwa upande wa machifu hao, vijana hao wawili walikuwa miongoni mwa kundi la kuchemsha mtindi haramu ambao baada ya kuvamiwa na machifu, walijirusha kweney mto huo wakijaribu kuogelea ili kukwepa mkono wa sheria na hivyo ndivyo walikutana na umauti wao.

Lakini wanakijiji mashuhuda walikuwa na maoni tofauti. Walisema kuwa vijana hao walisukumwa mtoni kwa nguvu wakiwa wamefungwa pingu mikononi na kuzama kwani hawangeweza kuogelea mikono yao ikiwa imefungwa.

Familia za wawili hao ambazo zinazidi kulilia haki miaka 4 baadae zilisema kuwa wanaume hao wawili walikuwa marafiki ambao walijitafutia riziki kama wavuvi.

Maithya alikuwa amemaliza kidato cha nne mwaka wa 2019 na alikuwa akipata riziki kwa kufuga samaki ili ajiandikishe kwa kozi ya waendeshaji mimea katika mji wa Thika.

Kamau alimaliza Darasa la Nane mwaka wa 2017 na kufanya uvuvi ili kupata riziki, akiwa na mpango wa kujiunga na chuo kikuu cha mitaa kwa kozi ya uashi, familia hizo zilinukuliwa na jarida moja la humu nchini.