Vita vya maneno baina ya Wakenya na Wanigeria Twitter kuhusu umri wa marais

Wakenya walianza kuwashambulia Wanigeria kwa picha na memes za kukejeli kuhusu hali yao duni kwa mambo mbalimbali.

Muhtasari

• Wengine walitumia picha ya Tinubu akionekana mnyonge na kuilinganisha na ya Ruto akionekana mkakamavu.

KOT washambulia Wanigeria kwenye Twitter
KOT washambulia Wanigeria kwenye Twitter
Image: Screengrab

Taifa la Nigeria lilishiriki katika mchakato wa Kidemokrasia wikendi iliyopita kuchagua viongozi wao.

Katika uchaguzi huo, mapema wiki hii tume ya uchaguzi Nigeria ilimtangaza mkongwe Bola Tinubu kama rais mteule baada ya kupata kura Zaidi ya milioni nane dhidi ya washindani wake wakuu Peter Obi na Atiku Abukabar.

Uchaguzi huo ulikuwa unafuatiliwa pakubwa nchini Kenya, na baada ya Tinubu mwenye umri wa miaka 70 kutangazwa mshindi, vita vya maneno baina ya Wakenya waliokuwa wakiwakejeli wenzao wa Nigeria vilizuka.

Waenya wengi walionekana kuwashambulia vijana wa Nigeria kwa kufanya kile walikitaja kama “maamuzi mabaya” kwa kumchagua mzee kama rais wao, licha ya kuwa taifa hilo lina asilimia kubwa ya wapiga kura vijana.

Wakenya kwenye mtandao wa Twitter walibuni kauli mbiu chini ya alama ya reli #WhichKenyans na #KenyansVsNigerians wakiwashambulia Wanigeria ambao pia walifanya jitihada za kujibizana vikali.

KenyansVS Nigerians
KenyansVS Nigerians

Majibizano hayo yaliyoanza mapema Alhamisi yameteka mtandao wa Twitter nchini Kenya ambapo mpaka kufikia Ijumaa asubuhi, gumzo hilo lilikuwa linaongoza katika mada zinazozungumziwa kwenye mtandao huo.

Wakenya wengi walionekana wabunifu katika mashambuizi yao ya kejeli yaliyojawa utani mwingi, wakitumia kigezo cha umri baina ya rais Ruto wa Kenya na rais mteule wa Nigeria Tinubu wakisema vijana wa taifa hilo hawana usemi katika uchaguzi, huku pia wakijisifu kuwa walikuwa wanadhani Kenya ndilo taifa liko pabaya katika demokrasia kumbe wenzao wa Nigeria wamevurunda hata Zaidi.

Mmoja alipakia picha ya treni ikiwa imesheheni makuni ya watu wengine mpaka wameparamia juu na kando kwenye madirisha akisema kuwa hao ni vijana wa Nigeria waliokuwa wakielekea katika taifa jirani la Mali ili kuchaji simu zao.

Mwingine pia alipakia picha za Ruto na Tinubu akisema rais wa Kenya ni ‘head of state’ huku yule wa Nigeria ni ‘End of state’

Mtumizi mmoja kwa jina Victor UDA General ambaye alionekana kutoa mashambulizi hayo kwa wingi alipakia picha ya wazee wakongwe akiwatania Wanigeria kuwa hiyo ndio taswira ya vijana katika taifa lao.

Hata hivyo, Wanigeria pia walijibu, mmoja akisema kuwa mjadala huo hauna maana kwani wao walikuwa wanafikiria Kenya ni kijiji kimoja tu katika taifa la Ghana.