"Tom Mboya alikosea nani?" Sakaja avunja kimya kuhusu wizi wa bango la Tom Mboya

Gavana alihoji uhusiano wa mwanasiasa huyo wa zamani na masaibu yanayokumba nchi kwa sasa.

Muhtasari

•Sakaja alibainisha kuwa ingawa kuandamana sio hatia, uharibifu wa maeneo ya biashara na mali jijini haukufaa.

•Kufuatia hayo, alitangaza kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wale ambao walinaswa kwenye picha na video.

amekashifu kitendo cha wizi wa bango la Tom Mboya
Gavana Sakaja amekashifu kitendo cha wizi wa bango la Tom Mboya
Image: HISANI

Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja amelalamika kuhusu uharibifu uliofanyika wakati wa maandamano ya Azimio mnamo  siku ya Jumatatu, Machi 20.

Akizungumza na wafanyibiashara katika kaunti ya Nairobi siku ya Jumanne, gavana huyo wa muhula wa kwanza alibainisha kuwa ingawa kuandamana sio hatia, uharibifu wa maeneo ya biashara na mali jijini hakukufaa.

"Ni jambo la kusikitisha. Kama ni kuandamana, ni sawa kujieleza jinsi unavyosikia. Lakini kuingia kwa duka ya mtu, kuchukua simu, kupiga watu ngeta," alisema.

Sakaja alieleza kusikitishwa kwake na wizi wa bango la barabara ya Tom Mboya na jamaa aliyenaswa na kamera akiwa amelibeba mgongoni.

Alihoji kuhusu uhusiano wa mwanasiasa huyo wa zamani na masaibu yanayokumba nchi kwa sasa ili kustahili kitendo hicho.

"Mtu amekimbia na bango la barabara, nauliza kwani Tom Mboya alikosea nani sasa jameni? Tom Mboya ako chini," alisema.

Gavana huyo wa chama cha UDA alidokeza kuwa maandamano ya Jumatatu yaliambatana na visa vingi vya unyanyasaji, wizi na uharibifu wa mali ya umma na ya kibinafsi na akabainisha kuwa ni jambo la kusikitisha.

Kufuatia hayo, alitangaza kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wale ambao walinaswa kwenye picha na video wakifanya vile.

"Tumewaona. Tutafanya uchunguzi kutumia kamera. Lazima watatajiwa kortini kwa sababu haifai kuwa hivyo kuharibia mtu biashara yake," alisema.

Maandamano ya Azimio siku ya Jumatatu yaligeuka kuwa ghasia katika baadhi ya maeneo ya nchi ikiwemo jiji la Nairobi na Kisumu na kusababisha uharibifu wa maeneo kadhaa ya biashara na mali nyinginezo.

Siku ya Jumanne, kiongozi wa Azimio, Raila Odinga alitangaza kuwa muungano huo utaendesha maandamano ya kupinga utawala wa rais William Ruto mara mbili kwa wiki.

Akihutubia waandishi wa habari, Raila alitangaza kuwa watakuwa wakiingia barabarani kila Jumatatu na Alhamisi kila wiki.

Kivumbi kitaanza wiki ijayo.

“Katika awamu ya pili tutaanza maandamano Jumatatu na Alhamisi kuanzia wiki ijayo,” alisema.

Mnamo Jumatatu, Raila alikuwa ametangaza kuwa maandamano ya upinzani yangefanyika Jumatatu kila wiki.

Akizungumza katika eneo la Kamukunji Raila alisema maandamano ya kushinikiza serikali yalikuwa yaendelea kuafanyika kila siku ya Jumatatu hadi pale serikali ingetekeleza matakwa ya upinzani na wananchi.

"Tumeanza vita. Kila Jumatatu kutakuwa na mgomo. Kutakuwa na maandamano. Vita imeanza haitaisha mpaka wakenya wapate haki yao," Raila alisema