'Kunguni': Sonko aomba radhi kuandika vibaya jina la kijana mwenye uhitaji wa karo

Kwa ufafanuzi wa haraka, neno ‘Kunguni’ haswa katika mitaa ya Nairobi hutumika kurejelea magenge ya vijana wanaohangaisha watu kwa kuwaibia.

Muhtasari

• Lakini katika kuizungumzia hadithi yake, Sonko alikosea katika kuliandika jina la kijana huyo – Kinyumu – na kujipata ameandika ‘Kunguni’ badala yake.

Mike Sonko.
Mike Sonko.
Image: X

Mfanyibiashara mkwasi ambaye aliwahi kuwa gavana wa kaunti ya Nairobi Mike Sonko alijikuta katika wakati mgumu kwa kuburuzwa na mashabiki wake katika mtandao wa X baada ya kukosea katika kuliandika jina la kijana mmoja ambaye alikuwa na uhitaji wa karo kujiunga kidato cha kwanza.

Sonko alipakia hadithi ya kusikitisha ya kijana huyo kwa jina Julius Kinyumu ambaye alikuwa anazungumziwa kwa kuhadithia jinsi anaelekea kuona ndoto yake ya kuendelea na masomo ikididimia.

Lakini katika kuizungumzia hadithi yake, Sonko alikosea katika kuliandika jina la kijana huyo – Kinyumu – na kujipata ameandika ‘Kunguni’ badala yake.

“Baada ya masaibu ya kunguni Julius akiniombea msaada wa kumuona akijiunga na shule ya upili, jana tarehe 31 Januari 2024 nilifanikiwa kumpata kupitia kwa mwalimu wake mkuu wa shule ya msingi aliyepita, nina furaha amelazwa katika shule ya upili ya St Charles Lwanga Boys kitui,” Sonko aliandika.

Katika mtandao wa X, ukishachapisha kitu kuhariri ni vigumu, pengine iwe mtu umelipia huduma ya kuhariri ambayo imezinduliwa mwaka jana na mmiliki wa jukwaa hilo, Elon Musk.

Hata hivyo baada ya kugundua makosa yake, Sonko alirejea katika jukwaa hilo na kuandika ujumbe mwingine wa kuomba radhi kwa kujikwaa huko.

Mhisani huyo aliweka wazi kwamba alikosea kwa kuliandika vibaya jina la kijana huyo na kuomba radhi si tu kwa kijana mwenyewe lakini pia kwa familia yake.

“Hoja ya kusahihisha: Kwa kweli, jina la mwanafunzi ni Julius Kinyumu na si Julius Kunguni, kama ilivyoelezwa awali. Pole zangu kwa mvulana na wazazi,” Sonko alieleza.

Alienda mbele ya kueleza kwa bashasha kwamba aliweza kufanikisha ndoto ya kijana huyo kwa kumpeleka shuleni na kumlipia ad azote.

“Nimemlipia ada ya shule ya mwaka mmoja 48,000/=, ada ya bweni 5350/=, pesa ya mfukoni kwa mwezi 2000=, sare za shule pea mbili pamoja na viatu 17,300/=, sanduku la shule na vitu vingine muhimu 5300/= pamoja na 11k uwezeshaji wa usafiri ( fuel) iliyotumwa kwa mwalimu wake wa zamani ambaye alimsindikiza shuleni. Namtakia kila la kheri katika masomo yake na naomba ndoto zake zije kuwa kweli,” Sonko alisema.

Kwa ufafanuzi wa haraka, neno ‘Kunguni’ haswa katika mitaa ya Nairobi hutumika kurejelea magenge ya vijana wanaohangaisha watu kwa kuwaibia.