Karen Nyamu azungumzia kufukuzwa kutoka nyumba yake ya Runda kufuatia mizozo ya kodi

Jumanne, ilidaiwa kwamba madalali kadhaa walioandamana na maafisa wa polisi walifika nyumbani kwa Bi Nyamu na nia ya kumfukuza.

Muhtasari

•Karen Nyamu amepuuzilia mbali madai ya kufukuzwa nyumbani kwake katika mtaa wa Runda, Nairobi kutokana na mizozo ya malipo ya kodi.

•Katika majibu yake, mama huyo wa watoto watatu alionekana kuzika uvumi huo akisema kuwa jambo kama hilo kamwe haliwezi kumtokea.

Image: FACEBOOK// KAREN NYAMU

Seneta wa kuteuliwa Karen Njeri Nyamu amepuuzilia mbali madai ya kufukuzwa nyumbani kwake katika mtaa wa kifahari wa Runda, Nairobi kutokana na mizozo ya malipo ya kodi.

Mapema wiki hii, kulikuwa na ripoti mitandaoni zilizodai kwamba madalali kadhaa ambao waliandamana na maafisa wa polisi walifika nyumbani kwa seneta huyo wa UDA kwa nia ya kumfukuza.

Mwanablogu Simon Muthiora Mwangi, alishiriki video ya maafisa katika ambako alidai kuwa ni nyumbani kwa Karen Nyamu. Pia kulikuwa na video iliyomwonyesha seneta huyo akiwa amesimama na maafisa wa polisi.

"Kizaazaa katika Runda Graceline Villa huku dalali wakiandamana na maafisa wa polisi katika jaribio la kumfurusha Seneta wa kuteuliwa Karen Nyamu kutoka kwa makazi yake kwa madai ya mzozo wa kodi.

Vyanzo vya habari vinasema Bi Nyamu ana malimbikizo ya kodi yanayoendelea kwa miezi kadhaa,” Mwanablogu Simon Muthiora aliripoti siku Jumanne kupitia mtandao wa Facebook.

Kwa kweli, uvumi huo ulienea kama moto wa msituni ukizua wasiwasi miongoni mwa wafuasi wa mwanasiasa huyo aliyezingirwa na utata mwingi, ambao walipiga hatua ya kumjulia hali na kutaka thibitisho kuhusu madai hayo.

Mtumiaji wa tiktok ambaye aliashiria wasiwasi kuhusu hali ya seneta huyo alitaka kujua ikiwa ripoti hizo zilikuwa za kweli akiweka wazi kwamba aliumizwa na madai hayo.

“Prezzo nina huzuni. Wanasema unafungiwa nyumba. Tafadhali sema kitu tumeumia,” Mwanatiktok Monicah Wanjiru aliandika.

Katika majibu yake, mama huyo wa watoto watatu alionekana kuzika uvumi huo akisema kuwa jambo kama hilo kamwe haliwezi kumtokea.

“Hilo kamwe haliwezi kunitokea maishani, mama pumzika. Tumebarikiwa sana,” alisema.

Mtumiaji mwingine wa mtandao wa tiktok alimshauri seneta huyo kujipatia nyumba yake binafsi kufuatia madai ya kufukuzwa, naye akajibu;

“Wueh sipendi kujibu kila kitu ambacho mtu anajaribu kuja nacho kwa sababu nitaonekana najigamba. Lakini nina uhakika unajua mimi si kasichana kajinga,” alisema.

Seneta huyo wa kuteuliwa hata hivyo hakushiriki maelezo zaidi kuhusu madai hayo ya kufurushwa ambayo yalitokea mapema wiki ikidaiwa alikosa kulipa kodi.