“Mitihani ni muhimu lakini si ya dharura!” Babu aomba vyuo kuachilia ‘comrades’ kushiriki maandamano

Babu Owino alisema kwamba ndio mitihani ni ya maana katika maisha ya mwanafunzi lakini si ya dharura kwani inaweza ikasongeshwa mbele ili kuwapa wanafunzi fursa nzuri ya kujiunga na Gen Z wenzao kuandamana.

Muhtasari

• Maandamano ya vijana yameanza katikati mwa jiji la Nairobi huku mamia ya vijana wakijitokeza kwa wingi.

Babu Owino
Image: maktaba

Mbunge wa Embakasi Mashariki ambaye pia anajiita msemaji wa wanafunzi wa vyuo vikuu, Babu Owino ameomba vyuo vyote humu nchini ambavyo viliratibu mitihani yao kufanyika wiki hii kughairi ili kuwapa nafasi wanafunzi kushiriki katika maandamano.

Mbunge huyo kupitia ukurasa wake wa Facebook alisema kwamba wanafunzi wa vyuo vikuu wana kila haki ya kujiunga na wenzao katika kushiriki maandamano ya kupinga kupitishwa kwa mswada wa fedha.

Babu Owino alisema kwamba ndio mitihani ni ya maana katika maisha ya mwanafunzi lakini si ya dharura kwani inaweza ikasongeshwa mbele ili kuwapa wanafunzi fursa nzuri ya kujiunga na Gen Z wenzao mitaani kuandamana dhidi ya mswada huo.

“Hakuna mwanafunzi anayepaswa kufanya MITIHANI au CATS leo katika chuo au chuo kikuu chochote nchini Kenya. Wenzake lazima wajitokeze kwa idadi na kutetea mustakabali wao. Mitihani hiyo ni muhimu lakini si ya dharura,” Babu Owino alisema.

Maandamano ya vijana yameanza katikati mwa jiji la Nairobi huku mamia ya vijana wakijitokeza kwa wingi.

Vijana hao wanatarajia kufurika kwa idadi ya karibia watu milioni moja.