Zaidi ya 200 wapoteza kazi klabu inayohusishwa na MP Oscar Sudi ikifungwa rasmi

Mbunge huyo alisema hasara kubwa iliyotokana na uvamizi katika klabu yake aliyoiweka kwa Sh200 milioni, ilimlazimu kuifunga na kusitisha kandarasi za wafanyakazi wote.

Muhtasari

• Klabu hiyo ilifunguliwa mwezi Mei katika hafla iliyohudhuriwa na wabunge kadhaa wanaounga mkono chama tawala cha Kenya Kwanza.

KLABU YA TIMBA XO
KLABU YA TIMBA XO
Image: HISANI

Klabu ya starehe ya Timba XO mjini Eldoret sasa imetangaza kusitisha shughuli zake rasmi kufuatia kuvamiwa na kuharibiwa wiki jana wakati wa maandamano ya vijana wa Gen Z.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo kwenye People Daily, klabu hiyo inayohusishwa na umiliki wa mbunge wa Kapseret Oscar Sudi imelazimika kufunga rasmi na kuwatuma nyumbani Zaidi ya wafanyikazi 200.

Klabu hiyo ilifunguliwa mwezi Mei katika hafla iliyohudhuriwa na wabunge kadhaa wanaounga mkono chama tawala cha Kenya Kwanza.

Vijana hao waliokuwa wamejihami kwa mawe na silaha nyingine ghafi waliharibu kuta za vioo, madirisha na milango ya jengo hilo la ghorofa mbili ambalo pia lina sehemu ya kuosha magari.

Walikuwa wameandamana kutoka katikati ya mji wa Eldoret hadi klabu hiyo kabla ya kuiharibu katika tukio la mchana.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, baadhi ya vijana walibeba vitu vya bei ghali miongoni mwao seti za TV, jiko la gesi, viti na vileo. Mamia ya maafisa wa polisi waliotoka katika vitengo vya utawala na amri za kawaida walitazama drama iliyokuwa ikiendelea kwa mbali.

Mbunge huyo alisema hasara kubwa iliyotokana na uvamizi katika klabu yake aliyoiweka kwa Sh200 milioni, ilimlazimu kuifunga na kusitisha kandarasi za wafanyakazi wote.