"Hakuna rasta, minisketi, tumbo cut..!" Chuo Kikuu cha KeMU chatoa sheria kali kwa wanafunzi

Ni sharti wanafunzi wanaume waingize shati zao kwenye suruali.

Muhtasari

•Sheria hizo mpya zinakusudiwa kuwasaidia wanafunzi kuzoea uvaaji nguo na mwonekano ambao utakubalika katika nyanja mbalimbali za kazi na jamii.

•Sheria  hizo mpya kali zinatumika kwa wanafunzi wote katika chuo kikuu hicho ambacho kinafadhiliwa na Kanisa la Methodisti

jijini Nairobi.
Chuo Kikuu cha Kenya Methodist jijini Nairobi.
Image: MAKTABA

Chuo Kikuu cha Kenya Methodist (KeMU) kimetoa sheria mpya kali kuhusu mtindo wa mavazi na  nywele kwa wanafunzi wake.

Kulingana na notisi kwa wanafunzi iliyofikia Radio Jambo,sheria hizo mpya zinakusudiwa kuwasaidia wanafunzi kuzoea uvaaji nguo na mwonekano ambao utakubalika katika nyanja mbalimbali za kazi na jamii.

"Wanafunzi wote wanatakiwa kutii kanuni za uvaaji za chuo kikuu (kifungu cha 3.21) na kuvaa mavazi yanayofaa wakati wa masomo, wakati wa chakula katika ukumbi wa kulia chakula, na katika hafla zote za chuo kikuu," notisi hiyo iliyotolewa Januari 5 na kutiwa saini na mkuu wa wanafunzi Esther Mbaabu alisoma.

Mitindo iliyopigwa marufuku kwa wanafunzi wa kiume ni pamoja na rasta, nywele zilizosukwa, hereni, kofia madarasani na vesti zinazoonyesha kifua wazi. Pia ni sharti wanafunzi wanaume waingize shati zao kwenye suruali, 

Wanafunzi wanawake hawataruhusiwa kuvalia shati fupi  zinazoonyesha kitovu na tumbo zao (tumbo cut), shati zinazoonyesha mgongo, nguo fupi zisizofikia magoti  (miniskirts) na nguo zenye mkato uliopita magoti.

Pia wamekatazwa kuvaa suruali zinazowabana, nguo zinazoonyesha sehemu kubwa ya shingo na zinazoruhusu mtu kuona ndani.

Sheria  hizo mpya kali zinatumika kwa wanafunzi wote katika chuo kikuu hicho ambacho kinafadhiliwa na Kanisa la Methodisti

Wakenya ambao wamefikiwa na notisi hiyo wameendelea kutoa maoni mseto kuhusiana na hatua hiyo, baadhi wakikosoa usimamizi wa chuo hicho na kuwashtumu kwa kuwa wakali huku wengine wakiunga mkono sheria mpya.

Je, maoni yako ni yepi kuhusiana na kanuni mpya za mavazi na nywele kwa wanafunzi wa chuo kikuu cha Methodist?