Itumbi ajawa bashasha baada ya rafiki yake Jacque Maribe kupata kazi kubwa serikalini

Maribe aliteuliwa kuwa mkuu wa mawasiliano katika wizara ya utumishi wa umma inayoongozwa na Waziri Moses Kuria.

Muhtasari

•Dennis Itumbi mnamo siku ya Jumapili alimpongeza rafiki yake Jacque Maribe baada ya kupata kazi nzuri serikalini.

•Huku akimpongeza rafiki yake huyo kwa jukumu jipya alilokabidhiwa, Itumbi alimwomba Mungu ambariki anapoanza kazi hiyo.

akimsindikiza Jacque Maribe nje ya Mahakama ya Milimani mnamo Februari 9, 2024.
Dennis Itumbi akimsindikiza Jacque Maribe nje ya Mahakama ya Milimani mnamo Februari 9, 2024.
Image: DOUGLAS OKIDDY

Mwanahabari na mtaalamu wa kidijitali Dennis Itumbi mnamo siku ya Jumapili alimpongeza rafiki yake Jacque Maribe baada ya kupata kazi nzuri serikalini.

Maribe ambaye hivi majuzi aliondolewa mashtaka katika kesi ya mauaji ya Monica Kimani aliteuliwa kuwa mkuu wa mawasiliano katika wizara ya utumishi wa umma, utendakazi na usimamizi wa utoaji huduma ambayo inaongozwa na Waziri Moses Kuria.

Huku akimpongeza rafiki yake huyo kwa jukumu jipya alilokabidhiwa, Itumbi alimwomba Mungu ambariki anapoanza kazi hiyo.

"Hongera Jacque Maribe- Mungu akubariki unapohudumu," Itumbi aliandika kwenye mtandao wa Facebook.

Pia alimshukuru waziri Moses Kuria kwa uteuzi huo akisema, " Asante Waziri Mhe CS Moses Kuria kwa kusimama na Kizazi, tafadhali endelea kufanya mema na kunyoosha mkono wako."

Maribe aliondolewa mashtaka katika kesi ya mauaji ya Monica Kimani mnamo Februari 9, 2024, na Jaji Grace Nzioka wa Mahakama ya Milimani kwa kukosa ushahidi.

Kulingana na Jaji Nzioka, shtaka lililowasilishwa dhidi ya Maribe halikuwekwa ipasavyo.

"Ni maoni yangu kwamba shtaka lililoletwa dhidi ya mshtakiwa wa pili halikuwa shitaka sahihi," alisema.

Muda mfupi tu baada ya Maribe kuondolewa mashtaka mwezi uliopita, Itumbi aliandika taarifa ndefu kusherehekea uamuzi wa mahakama.

Katika taarifa yake, Itumbi alisema anahisi amethibitishwa kuwa sahihi baada ya mashtaka yote dhidi ya mwanahabari huyo wa zamani kuondolewa.

Alisisitiza kuwa Maribe hakumuua marehemu mfanyabiashara huyo mwaka wa 2018 na akamshtumu mkuu wa upelelezi wa zamani kwa kumburuta hadi kwenye kesi hiyo.

“Jacque Maribe yuko HURU! Maribe HAKUMUUA Monica. Daaamn! Ninahisi kuthibitishwa sahihi!,” Itumbi aliandika kwenye mtandao wa Facebook.

Aliongeza, "Imekuwa miaka SITA, safari ya vivuli, ambapo minyororo isiyo ya haki ilitafuta kufunga roho ya rafiki mkubwa, haiba ya kupendeza, rafiki ninayemthamini sana. Leo, ukweli umefichua mwangaza wake, ukiondoa giza.

Mwanahabari huyo pia alitumia fursa hiyo kumtia moyo Bi Maribe kujitahidi kuinuka tena baada ya yale ambayo amepitia katika miaka sita iliyopita tangu kesi hiyo kuanza.

Pia alibainisha kuwa hajutii kusimama na wa mama huyo wa mvulana mmoja katika kipindi chote cha kesi hiyo iliyochukua miaka sita.