Siasa zitakunyenyekeza! Karen Nyamu ajicheka alivyolambishwa sakafu katika uchaguzi wa Nairobi

Nyamu alikumbuka alivyokuwa na matumaini ya kushinda kiti hicho kabla ya ndoto yake kukatizwa.

Muhtasari

•Nyamu alikuwa miongoni mwa wanasiasa  walioonyesha nia ya kuwa mwakilishi wa wanawake Nairobi mwaka wa 2017 lakini akashindwa vibaya.

•Alikumbuka jinsi washindani wake katika kura ya mchujo ya Jubilee, Rachel Shebesh na Millicent Omanga walivyomlambisha sakafu.

Image: INSTAGRAM// KAREN NYAMU

Seneta wa kuteuliwa Karen Nyamu amekumbuka mara yake ya kwanza kuwania kiti cha kisiasa nchini Kenya.

Nyamu alikuwa miongoni mwa wanasiasa wengi walioonyesha nia ya kuwa mwakilishi wa pili wa wanawake wa kaunti ya Nairobi mwaka wa 2017 lakini alishindwa vibaya wakati wa uteuzi wa kilichokuwa chama tawala, Jubilee.

Siku ya Alhamisi, seneta huyo wa UDA alikumbuka jinsi alivyokuwa na matumaini makubwa ya kushinda kiti hicho kabla ya ndoto yake kukatizwa na kuzikwa ghafla katika hatua ya mapema ya kura ya mchujo.

"Yaani hapa nilikua najua mimi ndio next mwakilishi wa wanawake ajaye. Wapinzani wangu nilikua nawahurumia tu ni vile nilikuwa niwashinde na mbali sana😂😂😂 nikikumbuka nacheka🤣," Karen alisema.

Wakili huyo aliambatanisha ujumbe huo na picha yake ya kumbukumbu akiwa kwenye mahojiano ya televisheni.

Alikumbuka jinsi washindani wake katika kura ya mchujo ya Jubilee, Rachel Shebesh na Millicent Omanga walivyomlambisha sakafu.

"Zile Kura Shebesh alinishinda nazo!!!! Nimenyenyekea milele🙌🏽😂😂 Kati ya wagombea 11 nilishika nafasi ya 3 kwa kura 46,000. Shebesh alikuwa ameshinda kwa kura 119,000. Omanga alikuwa wa 2 kwa kura 65,000," alisema.

Mwanasiasa huyo hata hivyo alidokeza kwamba anaamini kulikuwa na mchezo mbaya ambao ulichezwa katika uteuzi huyo.

"Marafiki zangu, siasa zitakufanya unyenyekee," alisema.

Nyamu hakukata tamaa katika siasa licha ya kushindwa vibaya katika uchaguzi wa 2017. Mwaka jana, alionyesha nia ya kuwa seneta wa Kaunti ya Nairobi kwa tikiti ya UDA kabla ya kuombwa kumuachia askofu Margaret Wanjiru.

Chama cha UDA hata hivyo kilimteua kama seneta baada ya kutwaa ushindi wa urais katika uchaguzi wa Agostui mwaka jana.

Mapema mwaka huu, Karen Nyamu alidokeza kuhusu mpango wake wa kuwania ugavana wa Nairobi katika siku za usoni.

Mwezi Machi, wakili huyo aliyezingirwa na drama si haba alichapisha picha yake akiwa nje ya ofisi ya gavana wa Nairobi na kuambatanisha na ujumbe ulioashiria anatazamia kuchukua wadhifa huo siku moja.

"Kanairo ipo siku! Habari ya asubuhi," aliandika.

Kama kawaida, Wakenya watumizi wa mitandao walijumuika chini ya chapisho hilo kutoa maoni kuhusu taarifa ya mwanasiasa huyo.

Aliyekuwa gavana wa kaunti ya Nairobi, Mike Sonko ni miongoni mwa mamia ya wanamitandao ambao walitoa maoni. Sonko alichukua fursa hiyo kumshauri Bi Nyamu huku akimwambia itakapofika wakati wake kuwania, amchukue mzazi mwenzake Samuel Muchoki almaarufu Samidoh kama mgombea mwenza.

"Ndio, na Samidoh akuwe naibu wako ikue kanairo ya Mugithi," alimwambia.

Nyamu hata hivyo hakujibu ujumbe wa gavana huyo wa zamani. Baadhi ya wafuasi wake wengine pia walimtia moyo kupigania nafasi hiyo ya uongozi siku za usoni huku wengine wakimkatiza tamaa.