Karen Nyamu ampa Edday Nderitu heshima yake, amtambua kama mke wa kwanza

Seneta huyo amevunja kimya baada ya familia ya Samidoh kusafiri kwenda Marekani.

Muhtasari

•Samidoh alichapisha picha yake na mkewe Edday Nderitu, watoto wao watatu na bosi wa kampuni inayoaminika kufadhili safari hiyo wakiwa katika uwanja wa ndege wa JKIA.

•Mwanamtandao  alimuuliza seneta huyo wa ni lini Samidoh anapanga kumpeleka kwa safari.

Edday Nderitu, Karen Nyamu, Samidoh
Image: HISANI

Siku ya Jumatatu, staa wa nyimbo za Mugithi Samuel Muchoki almaarufu Samidoh alifichua kuwa familia yake ilikuwa ikisafiri.

Baba huyo wa watoto watano alichapisha picha yake na mkewe Edday Nderitu, watoto wao watatu na bosi wa kampuni inayoaminika kufadhili safari hiyo wakiwa katika uwanja wa ndege wa JKIA.

"Safari ya Samburu," aliandika chini ya picha hiyo ambayo alichapisha kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Facebook.

Kama ilivyotarajiwa, mamia ya wanamitandao walimiminika chini ya chapisho hilo kutoa maoni tofauti huku baadhi yao hata wakimvuta mzazi mwenzake Samidoh, Karen Nyamu kwenye mazungumzo.

Kundi jingine la wanamitandao lilikimbia kwenye ukurasa wa seneta huyo wa kuteuliwa kumjulisha kuhusu maendeleo hayo mapya.

"Amka watu wanaenda samburu ma’am," mtumizi mmoja wa Facebook alimwandikia Nyamu kwenye ukurasa wake.

Katika jibu lake, mama huyo wa watoto watatu alifichua mahali ambako familia ya mzazi huyo mwenzake ilikuwa ikielekea. Aidha, alimtambua mkewe Samidoh, Edday Nderitu kama mke wa kwanza.

"Ni USA si Samburu lol na mzee hajaenda alikuwa anazindikisha 1st lady na watoto," alijibu.

Kwenye Instagram, mwanamtandao mwingine alimuuliza seneta huyo ni lini Samidoh anapanga kumpeleka kwa safari.

"Huoni wamepostiwa na kumpeleka out nyinyi ni lini? Usijaribu kutuchanganya na za birthday au baby shower," shabiki alimuuliza.

Alijibu, " Si ungeuliza mwenye anatupeleka ndio ako na ratiba. Akikwambia ukuje uniambia."

Kwa muda mrefu, kumekuwa na mzozo unaodaiwa kuwa kati ya seneta Nyamu na Edday Nderitu kuhusu ni nani mke bora kwa Samidoh.

Mapema mwaka huu, Edday alimwandikia Samidoh ujumbe mrefu kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii akimuonya kwamba hayuko tayari kamwe kulea watoto wao katika ndoa ya wake wengi.

Hii ilikuwa baada ya mwanamuziki huyo kuonekana na Nyamu licha ya seneta huyo awali kudai uhusiano wao umefika mwisho.

Edday alimtaja Bi Nyamu kama mtu asiye na maadili na asiyeheshimu familia yake. Alidokeza kuwa takriban miaka mitatu iliyopita ya ndoa yake imejawa na maumivu na fedheha nyingi. Hata hivyo, alisema licha ya yote amebaki mwaminifu na ameendelea kuunga mkono kazi ya msanii huyo wa nyimbo za Kikuyu. 

"Umenifanya nionekane mjinga na kuchukulia ukimya wangu kuwa wa kawaida, nimekusaidia kuinua kipaji chako na kukuunga mkono kwa yote, lakini kitu kimoja nimekwambia na nasema hapa tena sitalea watoto wangu katika familia ya wake wengi," Edday alimwambia mwanamuziki huyo mwezi Februari.