Gachagua afichua sababu ya kumpiga Samidoh marufuku kwenda nje ya nchi

Gachagua alisema kuwa Samidoh ni afisa wa polisi na walimfungia kutoondoka nchini ili kwanza kupata mwafaka wa amani baina ya Nyamu na Nderitu.

Muhtasari

• Gachagua alisema sasa wako tayari kumuondolea marufuku kwa sababu angalau kumeonekana kuwa na amani na heshima baina ya Nyamu na Nderitu.

Samidoh amjibu Gachagua
Samidoh amjibu Gachagua
Image: Facebook

Naibu wa rais Rogathi Gachagua amefichua sababu ni kwa nini katika miezi ya hivi karibuni msanii wa mugithi ambaye pia ni afisa wa polisi Samidoh hajawahi fanya ziara yake ya kimuziki nje ya nchi.

Akizungumza hatika halfa ya kusherehea miaka 25 ya safari ya muziki ya mwanamuziki mkongwe Muigai wa Njoroge wikendi iliyopita, DP Gachagua alisema kuwa aligundua Samidoh alikuwa amekosekana sana katika kuleta utulivu miongoni mwa wake zake wawili Edday Nderitu na Karen Nyamu.

Kutokuwepo kwake karibu na kina mama wa watoto wake kuliendeleza uhasama mkali baina ya wawili hao na ili kupata Amani, Gachagua alifichua kwamba alihakikisha Samidoh anapigwa marufuku dhidi ya kusafiri nje ili kusuluhisha tofauti zilizopo kati ya Nyamu na Nderitu.

Hata hivyo, Gachagua alisema kuwa huenda marufuku hiyo ikaondolewa kwa kile alisema kuwa msanii huyo amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuleta mapatano kati ya Nyamu na Nderitu.

“Unajua Samidoh nilikuwa nimempiga marufuku dhidi ya kwenda ng’ambo sababu mambo yake yalikuwa yanakaa hivi hivi. Lakini sasa naona mambo yake ameyatengeneza, nimfungulie aanze kwenda ng’ambo sasa?” Gachagua aliuliza umati ambao ulijibu kwa mbwembwe.

“Samidoh ni kijana wetu na tunampenda, lakini tumekubaliana na sasa naona amepanga maneno yake na Amani na heshima sasa ziko. Ningesema asiende ng’ambo lakini unajua ni polisi wetu na mmesema tumfungulie aende aimbe huko, aimbie wazungu lakini asiwaambie mambo yetu ya hapa nyumbani.”

Hii si mara ya kwanza kwa DP kummulika Samidoh papo hapo juu ya mahusiano yake. Mnamo Januari mwaka huu, Gachagua alimgeuzia joto Samidoh, akisema anahitaji kuwadhibiti wanawake wake dhidi ya kusababisha drama nyingi.

"Si tunapenda huyu Samidoh na nyimbo zake, lakini kuna mahali anatuangusha. Sasa wewe Samidoh control hii watu wako," DP alisema huku kukiwa na vicheko vikali kutoka kwa waumini.