Samidoh amtambulisha vizuri mzazi mwenzake Karen Nyamu katika mazishi ya mpwa wake

Nyamu alikuwa amempeleka Samidoh kumzika mpwa wake aliyepatikana amekufa katika mazingira tatanishi.

Muhtasari

•Samidoh na Nyamu waliandamana kwenye mazishi ya kijana aliyepatikana amefariki nyumbani kwa mwimbaji maarufu wa Mugithi.

•Samidoh alijitambulisha kama mjomba wa marehemu kabla ya kumualika Nyamu kuwasalimia waombolezaji na kuwafariji.

wakati wa mazishi ya shemeji ya DP Rigathi Gachagua mnamo Februari 23, 2023.
Seneta Karen Nyamu na Samidoh wakati wa mazishi ya shemeji ya DP Rigathi Gachagua mnamo Februari 23, 2023.
Image: FACEBOOK// KAREN NYAMU

Staa wa Mugithi Samuel Muchoki almaarufu Samidoh ni miongoni mwa waombolezaji ambao walihudhuria mazishi ya mpwa wake, Geoffrey Mwathi Ngugi, ambaye alifariki katika mazingira tatanishi mnamo Februari 22.

Samidoh aliandamana na mzazi mwenzake, seneta Karen Nyamu na marafiki kadhaa kwenye hafla hiyo iliyofanyika Nakuru.

Alijitambulisha kama mjomba wa marehemu kabla ya kumualika Bi Nyamu kuwasalimia waombolezaji na kuwafariji.

"Kuja Mama Wairimu usalimie watu. Kuja usalimie watu kisha turejeshe kipaza sauti kwa MC,"  alisema mwimbaji huyo.

Nyamu alitumia fursa hiyo kuwafariki waombolezaji na kuwatia nguvu waweze kukabiliana na majonzi ya kumpoteza mpendwa wao.

"Mimi naitwa Karen Njeri.Kama mlivyosikia, mimi ni seneta. Leo nashirikiana na nyinyi katika siku hii ya huzuni. Hatutamlalamikia Mungu. Hivyo ndivyo Mungu alikuwa amepanga. Tukienda juu tutakutana naye," alisema.

Mwathi alipatikana akiwa amefariki mnamo Februari 22 na ripoti iliyoandikishwa katika kituo cha polisi iliashiria kwamba alijitoa uhai kwa kuruka  kupitia dirisha la nyumba ya mwimbaji mashuhuri wa Mugithi.

Hata hivyo, maswali chungu nzima yasiyo na majibu yameibuka kufuatia mazingira tatanishi ambayo yamezingira kifo cha Mwathi. Marehemu alikuwa ameandamana na mwimbaji maarufu wa Mugithi nyumbani kwake usiku wa kuamkia Februari 22, pamoja na watu wengine kabla ya kupatikana amefariki.

Takriban wiki mbili zilizopita, Karen Nyamu na  Samidoh walionekana pamoja kwenye hafla ya mazishi ya shemeji wa naibu rais Rigathi Gachagua, Nancy Muthoni katika eneo la Gatanga, kaunti ya Murang'a.

Baada ya mazishi, Bi Nyamu alichapisha picha kadhaa za hafla hiyo  kwenye kurasa zake mbalimbali za mitandao ya kijamii.

Kati ya picha alizochapisha ni pamoja na moja ya mzazi mwenzake Samidoh akitoa hotuba yake kwenye hafla hiyo na nyingine inayoonyesha wakiwa wamekaa karibu na kuonekana kufurahia muda pamoja.

Siku moja baadaye, mkewe Samidoh, Edday Nderitu alimpa onyo mwimbaji huyo akimjulisha kuwa hayuko tayari kulea watoto wao katika ndoa ya wake wengi.

Kupitia taarifa ya uchungu kwenye ukurasa wake wa Facebook, mama huyo wa watoto watatu alimkashifu seneta huyo wa kuteuliwa akimtaja kama mtu asiye na maadili na asiyeheshimu familia yake.

"Nimemuomba Mungu kila siku anipe nguvu ya kukuombea lakini leo sina la kumwambia Mungu juu yako, umeniburuta na kuniweka mimi na watoto wangu kwenye bahari ya uchungu upate kukumbuka hili," Edday alimwandikia Samidoh.

Edday alidai kuwa mzazi mwenza wa mumewe, Karen Nyamu, anamzidi umri kwa miaka kumi, sababu nyingine ya kufanya akatae awe mke mwenzake.

Alibainisha kuwa ndoa yake ilikuwa nzuri siku za awali kabla ya mtu wa tatu kuingia ndani yake takriban miaka mitatu iliyopita.

"Imekuwa miaka 15 kamili ya ndoa iliyojaa panda shuka, ilikuwa mwanzo mdogo ambapo kidogo ilikuwa ya kutosha kwetu, kwa miaka mitatu iliyopita imekuwa maumivu,"