Karen Nyamu ajitambulisha kama bikira baada ya mavazi yake kukosolewa

Shabiki alikosoa gauni la Karen Nyamu akidai "Hilo gauni ni la wamama."

Muhtasari

•"Haruhusu maoni yao kumkengeusha kutoka kwa kusudi la Mungu kwa maisha yake. Muwe na Jumapili yenye baraka," aliandika.

•Nyamu ambaye hakuonekana kusumbuliwa na maoni hayo kwa kejeli alijibu "Wakati mwingine nitavaa ya bikira kama mimi."

Image: INSTAGRAM// KAREN NYAMU

Siku ya Jumapili, seneta wa kuteuliwa Karen Nyamu alijiandikia maneno mazuri kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Instagram.

Katika chapisho hilo, mama huyo wa watoto watatu alizungumzia jinsi anavyodhamiria kutimiza kusudi la Mwenyezi Mungu kwake kiasi kwamba maneno ya watu wenye lengo la kumuangusha chini hayamsumbui kamwe.

"Haruhusu maoni yao kumkengeusha kutoka kwa kusudi la Mungu kwa maisha yake. Muwe na Jumapili yenye baraka," aliandika.

Mwanasiasa huyo aliambatanisha ujumbe huo na picha yake akiwa na kiongozi wa wengi katika bunge la kitaifa, Kimani Ichung'wa.

Pichani, wawili hao walionekana wakipiga gumzo jukwaani huku furaha tele ikiwa imeandikwa kwenye nyuso zao. Ichung'wa alikuwa amevalia suruali ya jeans ya rangi ya buluu, shati yenye masanduku na koti lisilo na mikono huku Karen Nyamu akiwa amevalia gauni refu la rangi ya manjano.

Katika sehemu ya maoni, mtumizi mmoja wa Instagram alikosoa gauni lake huku akidai "Hilo gauni ni la wamama."

Nyamu ambaye hakuonekana kusumbuliwa na maoni hayo kwa kejeli alijibu "Wakati mwingine nitavaa ya bikira kama mimi."

Shabiki mwingine alimuonya mzazi mwenzake, Samidoh baada ya kuona muungano mzuri kati yake na Kimani Ichung'wa.

"Samidooo samido samidoo, nimekuita mara ngapi?? Hii karibu inaenda," nikita_ndungu alisema kwenye chapisho hilo.

Seneta huyo wa UDA alijibu, "Si rahisi."

Karen Nyamu na Samidoh wamekuwa kwenye mahusiano kwa muda mrefu na tayari wana watoto wawili pamoja. Mkewe Samidoh, Edday Nderitu hata hivyo amekuwa akipinga suala la mume wake kuwa na wake wengi.

Takriban miezi miwili iliyopita, Edday alimwandikia Samidoh ujumbe mrefu kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii akimuonya kwamba hayuko tayari kamwe kulea watoto wao katika ndoa ya wake wengi. Hii ilikuwa baada ya mwimbaji huyo kuonekana na Nyamu licha ya seneta huyo awali kudai uhusiano wao umefika mwisho.

Edday alimtaja Bi Nyamu kama mtu asiye na maadili na asiyeheshimu familia yake. Alidokeza kuwa takriban miaka mitatu iliyopita ya ndoa yake imejawa na maumivu na fedheha nyingi. Hata hivyo, alisema licha ya yote amebaki mwaminifu na ameendelea kuunga mkono kazi ya msanii huyo wa nyimbo za Kikuyu. 

"Umenifanya nionekane mjinga na kuchukulia ukimya wangu kuwa wa kawaida, nimekusaidia kuinua kipaji chako na kukuunga mkono kwa yote, lakini kitu kimoja nimekwambia na nasema hapa tena sitalea watoto wangu katika familia ya wake wengi," Edday alimwambia mwanamuziki huyo mwezi Februari.