"Nimechoka!" Samidoh azungumzia kumtunga mimba mkewe na Karen Nyamu tena

Mwimbaji huyo tayari ana watoto watano na wanawake wawili tofauti.

Muhtasari

•Mwimbaji huyo wa Mugithi ana watoto watatu na mke wake Edday Nderitu na wawili na mpenziwe, seneta Karen Nyamu.

•Wiki chache zilizopita, Nyamu alimsifia mwimbaji huyo kama baba mzuri na kuweka wazi kuwa anastahili watoto wengi.

Samidoh na bintiye
Image: HISANI//

Mwimbaji wa nyimbo za Mugithi Samuel Muchoki almaarufu Samidoh amedokeza kwamba amefunga ukurasa wa kupata watoto.

Samidoh ambaye tayari ana watoto watano na wanawake wawili tofauti ameweka wazi kuwa amechoka kuongeza wengine zaidi.

Alifichua hayo baada ya shabiki kumuuliza ni lini anapanga kuongeza mtoto.

"Kweli mkuu, tunaongeza mtoto lini?" Mtumizi wa Facebook alimuuliza.

Bila kusita alijibu, "Nimechoka!"

Mwanamuziki huyo anayeimba kwa lugha ya Kikuyu ana watoto watatu na mke wake Edday Nderitu na wawili na mpenziwe, seneta Karen Nyamu.

Wiki chache zilizopita, Nyamu alimsifia mwimbaji huyo kama baba mzuri na kuweka wazi kuwa anastahili watoto wengi. Alitoa kauli hiyo wakati akisherehekea siku ya kuzaliwa ya bintiye Edday Nderitu, Neriah Muchoki.

“Sawa kutokana na mahitaji ya umma hehehe. Baba mzuri anastahili watoto wengi. Heri ya kuzaliwa Neriah Muchoki,” alisema.

Seneta huyo wa kuteuliwa aliambatanisha ujumbe huo wa Facebook na picha zake, Samidoh na binti yao mdogo, Wairimu.

Mapema mwezi huu, Samidoh na  Edday waliandaa karamu kubwa kwa ajili ya kuadhimisha siku ya kuzaliwa ya binti yao Neriah.

Kupitia kurasa zake mnamo siku hiyo maalum, Edday alimtakia baraka bintiye na kumhakikishia uwepo wake katika maisha yake.

"Umepamba maisha yetu kwa mwaka mzima sasa, ulikuja katika maisha yangu nilipokuhitaji sana, wewe ni baraka kwa familia yetu, ukue katika hekima na kimo. Mungu akulinde na mabaya yote," alimwandikia bintiye.

Licha ya drama nyingi zilizozingira ndoa yao ya zaidi ya mwongo mmoja, wawili hao walionyesha mahaba mazito wakimsherehekea binti yao. Video zilizochukuliwa wakati wa karamu ya kuadhimisha siku ya  kuzaliwa  ziliwaonyesha wazazi wenza hao wawili wakicheza densi na kuburudisha wageni pamoja

Mwezi Februari, mama huyo wa watoto watatu alimwandikia Samidoh ujumbe mrefu kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii akimuonya kuwa hayuko tayari kulea watoto wao katika ndoa ya wake wengi.

Edday alidokeza kuwa takriban miaka mitatu iliyopita ya ndoa yake imejawa na maumivu na fedheha nyingi. Licha ya yote, anasema, amebaki mwaminifu na ameendelea kuunga mkono kazi ya mwanamuziki huyo.

"Nimebaki mwaminifu kwako bila kujali kudharauliwa, kudhalilishwa na kutukanwa kwenye mitandao ya kijamii, umenifanya nionekane mjinga na kuchukulia ukimya wangu kuwa wa kawaida, nimekusaidia kuinua kipaji chako na kukuunga mkono kwa yote, lakini kitu kimoja nimekwambia na nasema hapa tena sitalea watoto wangu katika familia ya wake wengi," alisema kwa uchungu.