Kenya yasajili idadi kubwa ya maambukizi ya Covid-19 kwa siku

Kenya  siku ya Ijumaa ilisajili idadi ya juu zaidi ya maambukizi ya virusi vya Covid-19 na kuzua hofu zaidi kuhusu maambukizi ya virusi hivyo.

Taifa kwa mara ya kwanza lilisajili jumla ya visa vipya 1,554 vya maambukizi ya korona chini ya saa 24 kutoka sampuni 9,389. Chini ya saa 24 Kenya pia ilisajili vifo 14 na kufikisha jumla ya watu 1,441 waliofariki kutokana na Covid-19 nchini Kenya.

Tangu kisa cha kwanza  cha Covid-19 kuthibitishwa Kenya mwezi Machi idadi ya maambukizi iliyotangazwa siku ya Ijumaa imefikisha jumla ya visa 81,656 vya maambukizi ya Covid-19 nchini Kenya.

 

Tawimu za wizara ya afya zaonyesha kuwa takriban sampuni 870,950 zimechukuliwa kufikia sasa.

Kati ya visa vilivyothibitishwa siku ya Ijumaa 1,526 ni raia wa Kenya huku 28 wakiwa raia wa kigeni, 950 ni wanaume huku 604 wakiwa wanawake.

Mtoto wa miezi mitano ndiye wa umri mdogo zaidi kuambukizwa huku mwenye umri wa juu zaidi akiwa na miaka 97.

Wizara ya afya pia imesema watu 1,200 wamelazwa katika hospitali mbali mbali nchini kutokana na makali ya korona huku wengine 7,521 wakiendelea kupokea matibabu wakiwa nyumbani.

Wagonjwa 72 wako katika vyumba vya wagonjwa mahututi, 41 wamewekwa katika mitambo ya kuwasaidia kupumua huku wengine 30 wakiwa kwenye oksijeni.

Visa hivyo vimesambaa katika maeneo mbali mbali kama ifuatavyo: Nairobi 546, Mombasa 159, Kilifi 153, Kiambu 96, Kericho 68, Meru 45, Kisumu 44, Nakuru 37, Bomet 33, Kakamega 32, Machakos 30, Kajiado 29, Nyandarua 27, Busia 25, Nyeri 25, Kisii 24, Uasin Gishu 22, Siaya 18, Lamu 16, Murang’a 15, Laikipia 14, Kitui 13, Samburu 12, Taita Taveta 11, Isiolo 10, Trans Nzoia 9, Bungoma 7, Nandi 6, Embu 6, Makueni 5, Turkana 4, Kwale 4, Vihiga 3, Homa Bay 2, Marsabit 2, Baringo 1 na Nyamira 1.