Covid-19: hospitali zaagizwa kutotoza ada za PPE

Muhtasari

• Kemsa inashikilia maelfu ya PPE katika magala yake.

• Inagarimu kati ya shilingi 21, 000 na 50,000 kila siku kupokea matibabu ya Covid-19.

Mhudumu wa afya akiwa amevalia mavazi rasmi ya kujikinga dhidi ya COVID-19. (Picha: MAKTABA)
Mhudumu wa afya akiwa amevalia mavazi rasmi ya kujikinga dhidi ya COVID-19. (Picha: MAKTABA)

Bunge la kitaifa limeidhinisha pendekezo la kamati ya bunge ya afya kuzitaka hospitali za umma kutowatoza wakenya gharama za vifaa vya kujikinga dhidi ya virusi vya covid-19 wanapolazwa.

Kamati hiyo ya bunge chini ya uwenyekiti wa mbunge Sabina Chege ilikuwa imetaka serikali kupitia wizara ya afya kusambaza vifaa vya PPE vinavyohifadhiwa katika magala ya KEMSA ili kutumiwa na madaktari katika hospitali za umma.

Hatua hii itakuwa afueni kwa wakenya waliolazwa katika hospitalli mbali mbali za umma kutokana na makali ya Covid-19 baada ya bima za matibabu kukataa kugharamia matibabu ya ugonjwa huo kutokana na gharama za juu za matibabu.

Kulingana na takwimu katika sekta ya afya, itakugarimu takriban shilingi 21,000 kila siku kupata matibau ya Covid-19 ukiwa na dalili za kadri. Kwa wagonjwa waliolazwa katika vyumba vya wagonjwa mahututi inagarimu takriban shilingi 50,000 kila siku kupata matibabu.

Hospitali zote zikiwemo za umma zimekuwa zikitoza wagonjwa ada za mavazi rasmi ya kujikinga ada ambayo bunge lilitaka iondolewe.

Kemsa ina maelfu ya vifaa vya kujikinga katika magala yake baada kubainika kwamba mamlaka hiyo ilinunua vifaa hivyo kwa bei ghali na bila kufuata kanuni za ununuzi wa bidhaa za umma.

Sakata hiyo imepelekea kusimamishwa kazi kwa afisa mkuu mtendaji wa Kemsa Jonah Manjari na maafisa wengine wa ngazi za juu kwa madai ya kukiuka kanuni za ununuzi wa bidhaa za umma alipoidhinisha ununuzi wa vifaa hivyo.

Manjari tayari amedai kwamba alitishiwa maisha na baadhi ya watu wenye ushawishi mkubwa katika serikali kupeana zabuni za ununuzi wa vifaa hivyo.