Mbivu na Mbichi

Ruto huenda akawafedhehesha Raila na Uhuru baada ya ushindi wa Msambweni

Wapiga kura huko Matungu watamchagua mbunge wao mpya machi tarehe 4 mwaka ujao .

Muhtasari
  • Bader,  mshirika wa Ruto  alimshinda Boga kwa kupata kura 15,251 dhidi ya 10,444 za Boga  na kumaliza  miaka 13 ya Raila kutawala siasa  eneo bunge hilo la Pwani .
  •  Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Martin Andati  ameonya kwamba juhudi za kuirekebisha katiba sasasa zipo hatarini .
  •  Wagombeaji walioungwa mkono na Ruto pia walishinda wadi ya  Gaturi  ambapo  Esther Mwihaki wa  People’s Empowerment Party  alimshinda Rosemary Wakuthii wa Jubilee. Chama cha PEP  kinahusishwa na mshirika wa Ruto Mlima Kenya Moses Kuria

 

Naibu wa rais William Ruto na mshindi wa uchaguzi wa Msambweni Feisal Bader

Ushindi wa mgombeaji aliyeungwa mkono na naibu wa rais William Ruto katika uchaguzi mdogo wa Msambweni  umelemaza kasi  ya BBI na  vugu vugu zima la handshake .

 Ushindi huo wa mgombeaji huru  Feisal Bader  dhidi ya  mgombeaji wa ODM  Omar Boga aliyekuwa pia akipatwa jeki kutoka upande wa serikali  utawarejesha katika meza ya mikakati rais Uhuru kenyatta na mshirika wake Raila Odinga kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022 .

Bader,  mshirika wa Ruto  alimshinda Boga kwa kupata kura 15,251 dhidi ya 10,444 za Boga  na kumaliza  miaka 13 ya Raila kutawala siasa  eneo bunge hilo la Pwani .

 

Boga  alikuwa amewasilishwa kama mgombeaji wa handshake  akiungwa mkono na kambi za Raila na Uhuru . Uhuru wiki jana alikutana na Boga pamoja na gavana Hassan Joho katika kilichoonekana kama hatua ya rais kumuidhinisha .

 Kipute hicho kilipewa taswira ya mapambano kati ya wanaounga mkono na kupinga BBI huku Ruto akiongoza kundi lake la ‘hasla’ kumfanyia kampeni Bader .

Raila   hata alichukua hatua ya kulinganisha kura hiyo kama mizani ya kuamua  mshindi kati ya wanaopinga na kuunga mkono BBI .

" Uchaguzi huu utatumiwa kama majaribio kufahamu iwapo BBI itapita  au la . Iwapo ODM itashindwa hapa basi BBI itakumbana na matatizo’ Odinga alisema kuhusu uchaguzi wa Msambweni disemba tarehe 10 .

Ruto  hakujitokeza  binafasi kumfanyia kampeni Bader  lakii alikituma kikosi kizto cha wanasiasa wa mrengo wa tanga tanga  wakiongozwa na gavana wa Kwale Salim Mvurya .

 Wachanganuzi wa masuala ya kisiasa wanasema matokeo hayo sasa yametoa taswira ya hali ilivyo kuhusiana na hatma ya BBI.

 Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Martin Andati  ameonya kwamba juhudi za kuirekebisha katiba sasasa zipo hatarini .

" Hata bila uongozi thabiti wa kupinga marekebisho hayo wananchi wana uwezo mkubwa wa kuikataa BBI’ amesema Andati

" Wananchi yanaonekana wazi hajawapendezwa na masuala ambayo Raila na Uhuru wanayapa kipau mbele  na wanalazimisha kupitishwa kwa BBI’

 Ukumbi ufuatao wa makabiliano kati ya mirengo hiyo sasa ni katika maeneo bunge ya Matungu katika  kaunti ya Kakamega na Kabuchai  ,Bungoma  ambapo ODM italenga kuthibitisha tena ubabe wake katika siasa za magharibi .

 Wanaoungwa mkono na ODM chama kilichoundwa kutokana na  kura ya maamuzi ya mwaka wa 2005 watakabiliana na wagombeaji watakaosimamishwa na vyama  ANC,Ford Kenya na  wanaoungwa mkono na naibu wa rais William Ruto .

 Wapiga kura huko Matungu watamchagua mbunge wao mpya machi tarehe 4 mwaka ujao .

 Wagombeaji walioungwa mkono na Ruto pia walishinda wadi ya  Gaturi  ambapo  Esther Mwihaki wa  People’s Empowerment Party  alimshinda Rosemary Wakuthii wa Jubilee. Chama cha PEP  kinahusishwa na mshirika wa Ruto Mlima Kenya Moses Kuria . Ushindi wa Ruto uliendelea pia hadi katika wadi ya  Lake View ambako chama cha Jubilee kilishindwa . ushindi huo huenda ukawapa viongozi wa mrengo wa Hustler ari ya kutaka kujitoa Jubilee  kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.